Mratibu wa Taasisi ya Uringo Dkt. Ave - Maria Semakafu akitoa mada kuhusu Madai ya Mabadiliko kwenye Katiba na Mtandao wa Wanawake na Katiba leo Jumatano Novemba 8,2023 wakati wa Warsha ya Ujenzi wa Harakati katika kuhamasisha uongozi kwa wanawake, kukuza sauti zao na Ushiriki katika siasa na nafasi za uongozi kwenye Tamasha la 15 la Jinsia na Miaka 30 ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) linalofanyika katika viwanja vya TGNP Mabibo jijini Dar es salaam. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mratibu wa Taasisi ya Uringo Dkt. Ave - Maria Semakafu akitoa mada kuhusu Madai ya Mabadiliko kwenye Katiba na Mtandao wa Wanawake na Katiba
Mratibu wa Taasisi ya Uringo Dkt. Ave - Maria Semakafu akitoa mada kuhusu Madai ya Mabadiliko kwenye Katiba na Mtandao wa Wanawake na Katiba
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Imeelezwa kuwa kuendeleza mfumo wa Viti Maalum vya Ubunge kwa wanawake unaathiri wanawake kwani umejaa ubaguzi na udhalilishaji wa Kijinsia hivyo unapaswa kubadilishwa au kuondolewa kabisa.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Novemba 8,2023 na Mratibu wa Taasisi ya Uringo Dkt. Ave - Maria Semakafu wakati akitoa mada kuhusu Madai ya Mabadiliko kwenye Katiba , Mtandao wa Wanawake na Katiba wakati wa Warsha ya Ujenzi wa Harakati katika kuhamasisha uongozi kwa wanawake, kukuza sauti zao na Ushiriki katika siasa na nafasi za uongozi kwenye Tamasha la 15 la Jinsia na Miaka 30 ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) linalofanyika katika viwanja vya TGNP Mabibo jijini Dar es salaam.
“Tunahitaji usawa 50 kwa 50,tunataka wanawake wengi wajitokeze kushika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi. Kwa upande wa ushiriki wa wanawake kwenye siasa, waleteni wanawake kwenye jamii tuje tuwapigie kura badala ya kuchaguliwa na chama cha siasa",amesema Dkt. Semakafu.
Amesema Mtandao wa Wanawake na Katiba haukubali kwamba mfumo wa viti maalum uliopo sasa uendelee kutumika kama njia ya kupata uzoefu na kisha kupisha wanawake wengine wenye nia ya kuongeza uzoefu na ujuzi wa masuala ya siasa.
“Kwetu sisi Wanamtandao wa Wanawake, Katiba, Uongozi na Uchaguzi, tunaona pendekezo la kuendeleza Viti Maalum ambavyo sisi kama wadau tunaoathirika na mfumo huu uliopo ambao tunaona umejaa ubaguzi na udhalilishaji wa Kijinsia, tunashauri ubadilishwe au kuondolewa kabisa”,amesema Dkt. Semakafu.
Ameeleza kuwa kuendeleza mfumo wa Viti Maalum wa sasa ni kuijengea jamii imani kwamba wanawake bado hawana uwezo, uzoefu wala ujuzi wa masuala ya siasa kwamba hao walioko kwenye uwanda wa siasa tayari wanahitaji takriban miaka kumi ya kujenga uwezo huo ili kuwapisha wengine wanaowania kuingia kwenye uwanda wa siasa.
Aidha ameshauri wanawake washiriki kwenye mchakato wa katiba mpya “Tusikubali Mchakato wa Katiba Mpya uendelee bila ya ajenda ya mwanamke”.
“Bima ya Watoto imeondolewa tupo kimya, tunatakiwa tujadili, tujishirikishe. Watoto waliokuwa wanatibiwa kwa shilingi 50400/= hivi sasa hawapati huduma za matibabu kutokana na masharti mapya ya Bima za Afya. Hili suala la bima linatugusa sisi wanawake, sisi ni wauguzaji wa watoto, waume zetu.Tunaomba Tozo za simu zitumike kulipia bima za watoto na wazee wa TASAF, lakini pia tunataka kuona mtanzania yeyote ananufaika na rasilimali za nchi”,ameongeza Dkt. Semakafu.
Social Plugin