Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AGIZO LA WAZIRI PROF.MKUMBO LIFANYIWE KAZI IPASAVYO NA MAMLAKA ZINAZOHUSIKA

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb,)wakati alipozindua kitabu cha mwongozo wa uwekezaji Mkoani Tanga wenye kauli mbiu Wekeza Tanga kwa Uwekezaji Endelevu.

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii na Mbunge wa Jimbo la Mkinga (CCM) Dastan Kitandula akizungumza wakati wa kongamano hilo

MKUU wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano hilo
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajab Abdurhamani akizungumza wakati wa Kongamano hilo


Na Oscar Assenga,TANGA

NI Ukweli usiopingika kwamba kumekuwa na urasimu usio wa lazima katika mchakato wa uwekezaji ambao wakati mwengine unatajwa kwamba ndio chanzo cha kuwakatisha tamaa wenye nia ya kufanya hivyo.

Jambo hilo limekuwa likipelekea kukwamisha watu wenye nia ya dhati ya kuwekeza na hilo kubwa linatokana na urasimu ambao unadaiwa kufanywa na mamlaka zinazohusika kwenye mchakato huo.

Kwa kuliona hilo kwamba jambo hilo ni changamoto kubwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb,) analitoa kauli wakati alipozindua kitabu cha mwongozo wa uwekezaji Mkoani Tanga wenye kauli mbiu Wekeza Tanga kwa Uwekezaji Endelevu.

Prof.Mkumbo anakemea vikali urasimu unaofanywa na Mamlaka zinazohusika na Uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na kusababisha Serikali kukosa mapato yake ya msingi

Katika Taarifa hiyo Prof.Mkumbo anawaagiza viongozi wa Serikali ngazi za mikoa kuhakikisha wanaondoa changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa kutoka ndani na nje yaa nchi ambao wakiwekeza wanalipa kodi na kukuza uchumi.

Katika hatua nyengine anazitaka mamlaka zote zinazohusika kwenye mchakato wa uwekezaji ziondoe urasimu usio wa lazima kiasi cha kuwakatisha tamaa wawekezaji.

Anaeleza kuwa kongamano hilo linaashiria dhamira ya dhati ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kukuza uchumi nchini hivyo uzinduzi huu ni hatua muhimu katika safari ya kujenga taifa linalovutia wawekezaji kutoka pande zote duniani kuja kushirikiana na Mikoa yote nchini.

Prof. Mkumbo anasema kuwa mfumo imara wa mazingira wezeshi ya uwekezaji ndio uti wa mgongo wa Taifa lolote linalojinasibu katika kufufua na kuimarisha uwekezaji wenye ustawi.

“Katika kutengeneza fursa za ajira, kuimarisha miundombinu na kuinua ubora wa maisha kwa wananchi wake lakini pia Mamlaka za Serikali za Mitaa zitenge maeneo mahususi na kuyahodhi kwa ajili ya uwekezaji “Anasema

Anasema pia wahakikisha wanayaweka miundombinu yote muhimu na kuandaa mkakati wa mawasiliano ili kuongeza kasi ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo na mipango yote ya uwekezaji izingatie dhamira ya Serikali ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Awali akizungumza katika Kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba anasema kuwa lengo la uzinduzi wa muongozo wa uwekezaji ni kufungua fursa za kilimo, uchumi wa bahari, viwanda, utalii, usafiri, afya, elimu, huduma za fedha, uendelezwaji wa miji na uboreshaji wa maeneo ya michezo.

Kindamba ameongeza kuwa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (East African Crude Oil Pipeline) wenye thamani ya dola za kimarekani 3.5 bilioni ni ishara tosha ya dhamira ya Serikali yetu katika kuhakikisha nchi yetu inafanya uwekezaji mkubwa na wenye tija kwa Taifa na wananchi wa kizazi cha sasa na cha baadae.

Anasema kuwa uwekezaji uliofanywa katika kuboresha Bandari ya Tanga uligharimu kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni 429.1 ambapo kazi zilizofanyika zilikuwa ni kupanua gati na kuongeza kina na hivyo kuongeza uwezo na ufanisi wa Bandari hiyo.

Aliongeza ili kuhakikisha kwamba inaweza kukidhi ongezeko la shughuli inayoendelea ya ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki na shughuli nyingine za kibiashara, kiusafirishaji na kiuwekezaji. Bomba la mafuta linaloanzia Hoima nchini Uganda hadi chongoleani Tanga

Kongamano hilo limehudhuriwa na Waheshimiwa Mabalozi kutoka Rwanda, Burundi, Uganda na wengine kushiriki kwa njia ya mtandao, Naibu waziri Wizara ya Maliasiri na Utalii Mhe. Danstan Kitandula (Mb), Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Abubakar Kunenge, Mheshimiwa Nurdin Babu, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro pamoja na wakuu wa Wilaya, wabunge, makatibu tawala na wakurugenzi wa halmashauri.

Ndio maana tunasema kwamba kauli ya Prof.Mkumbo ifanyiwe kazi ipasavyo na mamlaka husika ili iweze kuleta tija kwa wawekezaji ambao wanakuja kuwekeza hapa nchini na wale wazawa na isipuuzwe.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com