Edwin Soko
Mwandishi wa habari na Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari za kupiga vita matukizi ya dawa za kulevya na uhalifu Tanzania (OJADACT) Edwin Soko, katika kuhakikisha wana habari wanakuwa salama kazini, atamwandikia barua Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, kumshawishi/kumuomba awasilishe Muswada Binafsi wa Ulinzi wa waandishi wa habari.
Soko alisema hayo jana kwenye kilele cha maadhimisho ya kimataifa ya kupinga dhuruma na ukatili dhidi ya waandishi wa habari Duniani.
Soko alibainisha wazi kuwa nia yake ni kuhakikisha muswada huo unawasilishwa bungeni kwa hati ya dharura ili sheria ya ulinzi wa waandishi wa habari ipatikane haraka na itumike kwenye kuwalinda waandishi wa habari kuanzia kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani 2024 na uchaguzi mkuu wa Mwaka 2025.
"Waandishi wa habari wamekuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu sana bila kuwa na ulinzi wa kisheria hali hiyo ni hatari kwa usalama wao", alisema Soko.
Pia aliongeza kuwa jambo hilo linawezekana kwa kuwa lipo kwenye Miongozo ya bunge hivyo wabunge wakielimishwa umuhimu wa jambo hilo wao ni rahisi kuwasilisha muswada binafsi.