MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Gissima Nyamo- hanga,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Novemba 24,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme nchini.
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Gissima Nyamo- hanga,akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 24,2023 jijini Dodoma kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme nchini.
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Gissima Nyamo- hanga,akijibu Maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme nchini leo Novemba 24,2023 jijini Dodoma.
Na.Mwandishi Wetu-DODOMA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limesema upatikanaji umeme kwa kipindi cha Septemba hadi Novemba mwaka huu imeimarika baada ya kuongeza zaidi ya Megawati 197 kwenye Gridi ya Taifa na kufanya upungufu wa umeme kushuka kutoka Megawati 410 hadi kufikia Megawati 213 hivyo kupunguza makali ya mgao wa umeme nchini.
Hayo yamesemwa leo Novemba 24,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Gissima Nyamo- hanga wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme nchini.
"Takribani megawati zaidi ya 197 zimeongezeka katika mfumo wetu wa gridi ya taifa ndani ya kipindi tajwa kutokana na juhudi mbalimbali za matengenezo ya mitambo, kuongezeka kwa upatikanaji wa gesi asilia kutoka TPDC, sambamba na upatikanaji wa mvua katika ukanda wa vituo vya kuzalisha umeme vya Nyumba ya Mungu,Hale na Pangani"amesema Mhandisi Nyamo- hanga
Mhandisi Nyamo- hanga amesema kuwa hali ya uzalisahaji umeme kwa kutumia vyanzo vya maji bado haujaimarika kutokana na mvua kuchelewa kunyesha katika mikoa ambayo huchangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji katika vituo vya kuzalisha umeme.
"Vyanzo hivyo ni pamoja na Mtera, Kidatu na Kihansi yaani katika mikoa ya Iringa, Mbeya,Tabora, Singida na Dodoma kwa sasa kumekuwepo na dalili ya mvua katika mikoa hiyo jambo ambalo linaashiria kuwepo kwa ongezeko la uzalishaji wa umeme katika vituo hivyo katika kipindi cha muda mfupi kutoka sasa"amesema
Hata hivyo amesema kuwa shirika linautaarifu umma kuwa mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo ya ukanda wa Pwani na Tanga na zile za mikoa ya kanda ya ziwa Victoria katika mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita na Kagera ni mvua ambazo mtiririko wake wa maji hauelekei viliko vyanzo vya umeme vya Mtera,Kidatu na Kihansi.
"Na hii ndo sababu hasa kuendelea kuwepo kwa mgao wa umeme pamoja na kwamba mvua zinazonyesha katika maeneo ya kanda hizo mbili "amesema
Vile vile,Mhandisi Nyamo- hanga amesema kuwa mvua hizo zinazoendelea kunyesha kwa wingi katika kanda hizo zimeleta athari katika miundombinu ya shirika na kuongeza makali ya upatikanaji wa huduma ya umeme kwa baadhi ya ya wateja.
Aidha amesema kuwa shirika linaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na upungufu huo wa umeme kwa kufanya matengenezo mitambo yake, kuongeza vyanzo zaidi vya kuzalisha umeme, kuongeza upatikanaji wa gesi asilia sambamba na kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme.
"Shirika linaendelea kusimamia kwa umakini zoezi la mgao wa umeme linaendelea hadi sasa ili kupunguza makali ya mgao nchini,"amefafanua
Pia amesema kuwa ili kuhakikisha ubora wa huduma kwa wateja unaongezeka shirika litaimarisha ukubwa wa kituo chake cha mawasiliano kwa wateja kwa kuongeza idadi ya watoa huduma wanaopokea na kujibu simu za wateja kutoka 65 hadi 100 ili kumudu ongezeko.
"Shirika linautaarifu umma kwamba hali ya upatikanaji wa umeme itaendelea kuimarika katika miezi ya usoni kutokana na kukamilisha matengenezo ya mitambo iliyokuwa na hitilafu. Kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi asilia, kukamilika kwa mradi wa Rusumo utakaotupatia megawati 27 na mradi wa bwawa la kufua umeme la mwalimu Julius Nyerere litakalokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2115”amesema Mhandisi Nyamo- hanga
Social Plugin