Na Deogratius Temba - Dar es salaam
MWANAHARAKATI mkongwe wa Haki za wanawake na usawa wa Kijinsia profesa Marjorie Mbilinyi ameitaka serikali kusimamia kikamilifu mgawanyo wa rasilimali za umma ili ziwanufaishe wananchi wote bila ubaguzi.
Akizungumza Leo Novemba 8,2023 wakati wa mdahalo wa Kifeminia, nyayo zetu, ndoto zetu, kwenye Tamasha la 15 la Jinsia na miaka 30 ya TGNP, jijini Dar es salaam, amesema kwamba, kwa kipindi cha miaka 30 ya uwepo wa TGNP,taasisi ilijitahidi kwa kiasi kikubwa kushinikiza mabadiliko ya kisera na kisheria ili kuondoa pengo la umaskini na ubaguzi katika kunufaika na rasilimali za umma.
“ Tukikumbuka mwaka 1990, tuliona uporaji wa rasilimali, madini, misitu, ulikithiri sana, makampuni makubwa yalikuja kutokana na sera ya ubinafsishaji. Wakati ule tulikuwa na deni kubwa la taifa, watu walikuwa wanaomba msahamaha, waliotukopesha walitoa masharti ya kusamehewa deni”,amesema.
“TGNP tulihakikisha tunafanya uchambuzi wa bajeti kwa mtazamo wa kijinsia, ili kubaini pengo na madhara ya deni la taifa kwa kijinsia. Tunataka kuona nafasi ya wananchi kushiriki moja kwa moja katika maamuzi, wananchi wote wanufaike moja kwa moja na mgawanyo wa rasilimali zetu. Hivi karibuni nafasi ya kutoa maoni na kusikilizana imeongezeka sana kutokana na ongezeko la vitendea kazi na nyenzo za kiteknolojia”, ameongeza
TAZAMA VIDEO HAPA PROF. MARJORIE AKIZUNGUMZA
Social Plugin