DKT. BITEKO AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA NORWAY


Na Mwandishi Maalum. 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo amekutana na kufanya  mazungumzo na Balozi wa Norway nchini, Mhe.Tone Tinnes ambapo mazungumzo yao yalijikita katika maeneo ya ushirikiano katika Sekta ya Nishati ikiwa mwaka huu nchi ya Norway imetimiza miaka 50 ya ushirikiano wake na Tanzania katika Sekta ya Nishati.

Katika mazungumzo hayo, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Dkt. Biteko alimweleza  Balozi Tinnes,  kuhusu maendeleo ya miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa Gesi ya Kusindika (LNG) ambayo majadiliano yake yamefikia ukingoni ambapo kampuni ya Equinor kutoka Norway ni moja ya wawekezaji kwenye mradi huo.

Aidha, alimueleza,  Mhe.Balozi kuhusu hatua nzuri  zilizofikiwa katika  mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unaotarajiwa kukamilika mwakani ambapo pia amemkaribisha kuutembelea mradi huo ili kuona maendeleo yake.

Vilevile, amemueleza kuhusu hatua za mafanikio ya utekelezaji miradi ya umeme vijijini ambapo amesema kuwa mwezi Juni mwaka 2024 kila Kijiji kitakuwa kimeunganishwa umeme.

Dkt. Biteko ameikaribisha Norway kushirikiana na Tanzania katika kuendeleza miradi ya umeme wa Maji ya Ruhudji na Rumakali kutokana na uzoefu mkubwa wa nchi hiyo katika miradi ya umeme wa maji kwani asilimia 80 ya umeme wa nchi hiyo unatokana na maji.

Viongozi hao pia wamezungumzia masuala ya Nishati Jadidifu ambapo Balozi wa Norway amemueleza Waziri Biteko kuwa kampuni nyingi kutoka nchi hiyo zina nia ya kuwekeza kwenye eneo hilo.

Pia ameipongeza Tanzania kwa hatua nzuri walizofikia katika usambazaji umeme na katika mradi wa LNG.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post