Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. BITEKO AZINDUA MASHINDANO YA SHIMMUTA *TPA, TAWA, NSSSF ZASHIRIKI*




Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amezindua mashindano ya Michezo ya shirikisho la Michezo la mashirika ya Umma,Taasisi na makampuni binafsi(SHIMMUTA)jijini Dodoma huku akimtaka Msajili wa Hazina nchini kuwasilisha maelezo ya kina kuhusu mashirika ambayo yameshindwa kushiriki mashindano hayo. 

Akizungumza leo November 17,2023 kwenye uzinduzi huo,Dk.Biteko ameeleza kuwa ni aibu kwa taasisi hizo za serikali kutoshishiriki mashindano hayo ambapo kati ya taaaisi na mashirika 248 ni 57 pekee ndiyo yameweza kushiriki.

"Kama tumekubaliana kufanya jambo fulani basi tulifanye, na kama tunaona halifai  basi bora tuliache, kuliko tunakubaliana kufanya kitu  halafu hatukifanyi; haiwezekani  viongozi wote hapa wanalalamika, Katibu Mkuu analalamika, Naibu Waziri analalamika na mimi nilalamike?, hapana sijaumbwa hivyo, sioni sababu yoyote ya kutamkika au ya kuandikika, kwamba kuna mashiriki ya umma 248 na hapa yapo mashirika 57 tu; haiwezekani." Amesisitiza Dkt.Biteko

Aidha, amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kuwaandikia barua Makatibu Wakuu wa Wizara ambao Taasisi zao hazijashiriki michezo hiyo, watoe maelezo kwanini hawajapeleka wafanyakazi kwenye mashindano hayo na yeye atashauri viongozi Wakuu wa Nchi, hatua za kuchukua.Vilevile, ameelekeza mashirika yote ya Umma yanayotakiwa kujiunga na SHIMMUTA kufanya hivyo.

Aawali, Mwenyekiti wa Kamati ya SHIMMUTA, Roselyne Massama amemweleza Naibu Waziri Mkuu kuwa wanakumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya muitikio mdogo wa Mashirika ya Umma kushiriki mashindano hayo jambo ambalo linazorotesha mashindano hayo.

Nao baadhi ya washiriki wa mashindano hayo wameeleza kuwa mashindano hayo ni muhimu kwani yanatoa nafasi ya kupumzisha akili baada ya kufanya kazi kwa muda mrefu hasa baada ya Serikali kuweka msukumo kwenye sekta ya Michezo kwa kukarabati viwanja . 

Afisa uhifadhi Mwandamizi  wa  Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA)Carlos Ernest amesema mashindano hayo yatadumisha uhusiano na taasisi mbalimbali na kwa upande wao mchezo mpira wa miguu wanafanya vizuri na upande wa netboli wamepoteza mechi 1 na wanafanya vizuri kujituma lakini kikubwa ni nidhamu ili kuhakikisha wanapata vikombe vyote.

"Mashindano haya ni huduma kwetu, ni muhimu kwetu kwa ajili ya kutuweka fiti, jeshi letu linahitaji uimara na utayari hivyo kuwa sehemu ya mashindano haya ni fursa kwetu, tunamshukuru uongozi Wetu kwa kujitoa kutuwezesha kushiriki hapa kwani kwa kufanya hivi tutaongeza ari ya kufanya kazi, " amesema

Naye Mwenyekiti wa timu ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSSF)Patrick Gandye amesema michuano hiyo ambayo ilianza tangu jumamosi yana umuhimu mkubwa kwa kuwasaidia  kujenga ukaribu na mashirika mengine ya Serikali na Taasisi .

"Kwa Taasisi ambazo hazijashirik inabidi wafanye hima waweze kushiriki kwenye haya mashindano ikiwemo taasisi binafsi pamoja na mashirika ya serikali, ni muhimu kwa kila mfanyakazi kuwa na afya njema kupitia Michezo na kupata muda wa kupumzika," Amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa timu ya Mamlaka ya bandari Tanzania (TPA)Raymond Nyarufunjo ameeleza mafanikio ya mashindano hayo kwa mwaka huu kuwa ni ya kipekee,yanavutia na kuongeza ari ya wengine kushiriki kwenye Michezo. 

Amesema wao kama watumishi wa Umma wanatumia nafasi hiyo kujijenga kimwili na kiakili na kwamba baada ya hapo kazi itaenda sawa huku akieleza kuwa TPA kwa mwaka jana walikuwa washindi wa pili na walifanya vizuri na kuwaahidi watanzania kuusubiri ushindi wao kwa mara nyingine. 

Nyarufunjo amesema,"Nawasihi Taasisi zingine ziweze kuleta wanamichezo wao kwa sababu mbali na kwamba tunabadilishana uzoefu pia michezo inasaidia kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari na saratani lakini pia kuimarisha uhusiano katika taasisi za umma,"amesema

Viongozi mbalimbali wamehudhuria Hafla ya Ufunguzi huo akiwemo Hamisi Mwinjuma, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Rosemary Senyamule, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Roselyne Massam Mwenyekiti wa SHIMMUTA.

Michezo hiyo ambayo mwaka huu imefikisha miaka 53 kutoka kuanzishwa kwake na Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere, imejumuisha Taasisi 57 na wanamichezo walioshiriki ni 3478 huku michezo inayoshindaniwa ikiwa ni 12.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com