Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akijibu hoja zilizoibuliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa hesabu zilizokaguliwa kwa Serikali Kuu na Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioisha 2022/2023.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiwa pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako wakifuatilia maoni ya Wabunge Bungeni leo tarehe 4 Novemba, 2023 wakati wa kikao kinachojadili Taarifa ya Kamati Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Heabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu hesabu zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC).
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema kamati maalum imeundwa kwa ajili ya kufuatilia fedha za michango ya wanachama wa Mfuko ya Hifadhi ya Jamii PSSSF na NSSF ambazo hazijawasilishwa na waajiri.
Akichangia Novemba 4, 2023 bungeni taarifa ya kamati za bunge zinazoshughulikia ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof.Ndalichako amesema katika ripoti ya CAG mfuko huo ulikuwa ukidai michango Sh. Bilioni 408 ambazo zilikuwa hazijakusanywa baada ya maelekezo ya Rais na kuzingatia hoja za CAG iliundwa kamati hiyo.
Amesema kamati hiyo imefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 200.6 kati ya TSh. Bilioni 408 na kusisitiza serikali itahakikisha fedha zilizobaki zinakusanywa.
Kuhusu michango ya wafanyakazi wa halmashauri, Profesa Ndalichako amesema pia kiliundwa kikosi kazi Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na tayari wameingia makubaliano na halmashauri 81 ambazo zina madai ya muda mrefu na zimewesha kuwakomboa wastaafu 1,425 kulipwa madai yao.
Aidha, Waziri Ndalichako amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF kufuatilia Halmashauri 103 ambazo hazijaweka makubaliano namna watakavyowasilisha michango wanayodaiwa kwa muda mrefu.
“Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI nitakukabidhi orodha ya Halmashauri ili fedha hizo zikusanywe tuweze kulipa mafao wastaafu wetu,” amesema.