Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) leo kimeendesha Kongamano la TEHAMA Arusha kwa mwaka 2023 ambalo limefanyika katika Kampasi ya Arusha kwa lengo la kuwakutanisha wadau wa TEHAMA ndani na nje ya Mkoa wa Arusha kujadiliana masuala mbalimbali kuhusu TEHAMA likiwa na kauli mbiu “Mabadiliko ya kidigitali katika kuendeleza shuguli za binadamu”.
Akizungumza katika Kongamano hilo Mkuu wa Chuo IAA, Prof. Eliamani Sedoyeka amesema Kongamano hilo limekuwa chachu katika kuibua vipaji kwa wanafunzi, kuonesha kazi zao za ubunifu na uvumbuzi katika TEHAMA, kuwakutanisha na wadau wa TEHAMA na kujadiliana namna ya kuwawezesha kuweka mazao ya ubunifu wao sokoni.
Aidha, Pro. Sedoyeka amesema katika kuendana na kasi ya Serikali katika uwekezaji kwenye TEHAMA, IAA imeendelea kuwekeza katika uboreshaji wa miundombinu na uanzishwaji wa mitaala bora ili kuweza kutoa wataalam wenye uwezo wataokakubalika sokoni na watakaotumia elimu na ujuzi wao kutatua changamoto katika jamii.
“Sisi kama Chuo tumewekeza katika miundombinu ya TEHAMA, mitaala na rasilimaliwatu; IAA kupitia Mradi wa HEET tunatarajia kujenga kituo cha kikubwa cha umahiri cha TEHAMA, ambapo mtu yeyote atakayehitaji suluhisho la changamoto yoyote ya TEHAMA atakuja IAA,” amesema Prof.Sedoyeka.
Akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA nchini, Mkurugenzi wa Huduma za Kiufundi Mhandisi. Jasson Ndanguzi amesema, Tume hiyo itaendelea kushirikiana na Vyuo vya elimu ya juu katika kufanya tafiti zinazoibua mwelekeo wa TEHAMA, zinazotatua changamoto za jamii, kuibua fursa za kiuchumi pamoja na kuiwezesha serikali kuandaa sera zinazoendana na wakati.
Mhandisi Ndanguzi ameipongeza IAA kwa kufanya makongamano ya TEHAMA na kuahidi kuwa Tume itaendelea kuwasaidia wabunifu wa mifumo ya TEHAMA hususani wanapofikia hatua ya kuipeleka mifumo yao sokoni kwa walaji ili watimize lengo la kuisaidia Jamii.
Naye Amidi wa Kitivo cha TEHAMA katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Edson Lubua amesema kongamano hili limekuwa likitoa motisha kwa wanafunzi na kuonesha thamani ya kazi za bunifu zao pale wanapozionesha kwa walaji ambao ni makampuni, waajiri na taasisi mbalimbali ambazo zinaweza kuwawezesha kufikia ndoto zao.
Said Hussein na wenzake watatu ni wanafunzi wa shahada ya usalama wa mtandao, ambao wamebuni mfumo maalum wa kutengeneza vitambulisho, unaoweza kutumika na taasisi mbalimbali, hivyo wametoa wito kwa wamiliki na wakuu wa taasisi kuwaunga mkono kwa kutumia mfumo huo ambao kwa sasa unatumika kutengeneza vitambulisho kwa wanafunzi wote wa IAA.
Pamoja na mfumo wa kutengeneza vitambulisho wametengezeza mifumo mingine mbalimbali waliyoionesha katika kongamano hilo ikiwemo mfumo wa utambuzi wa magonjwa katika mimea, mfumo wa utafutaji wa mafundi kupitia mtandao pamoja na mfumo wa utoaji wa taarifa katika taasisi kupitia mtandao.
Social Plugin