MAAFISA TARAFA NA WATENDAJI KATA SHINYANGA WAPEWA MAFUNZO...WAHIMIZWA KUIMARISHA UADILIFU , UKUSANYAJI MAPATO


Maafisa tarafa na watendaji wa kata Mkoani Shinyanga wametakiwa kuimarisha uadilifu na kusimamia kikamilifu suala zima la amani na ushirikiano baina yao na wananchi sambamba na kusimamia ukusanyaji wa mapato ndani ya mamlaka ya serikali za mitaa.

Hayo yamesemwa leo Novemba 30, 2023 na Afisa elimu Mkoa wa Shinyanga Dafroza Ndalichako wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa tarafa na watendaji wa kata waliopo ndani ya mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika kwa muda wa siku mbili kwenye ukumbi wa mikutano katika Chuo cha Ualimu Shinyanga (Shycom).

 Ndalichako amewasihi viongozi hao wa ngazi ya tarafa na kata kuyaishi yale waliofundishwa lakini pia kusimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato ya serikali kwa kutumia mifumo iliyowekwa.

“Wote ni mashahidi kuwa sehemu yoyoye ambayo haina amani na utulivu wananchi hawataweza kushiriki shughuli za maendeleo na hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi, hivyo nendeni mkaimarishe amani, utulivu na mshikamano lakini pia kasimamieni ukusanyaji wa mapato. Usimamizi wa mapato ndani ya mamlaka ya serikali za mitaa utaendelea kuwa kipaumbele cha serikali sambamba na matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato", amesema Ndalichako.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeleta fedha nyingi katika mamlaka ya serikali za mitaa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali hivyo ni wajibu wenu kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya maeneo yenu, mkasimamie na kufuatilia fedha za miradi zinazotolewa na serikali ili ikawe na tija kwa wananchi na kuondoa changamoto ya kukosa huduma”.

“Makusudio ya kutoa mafunzo haya kwenu kupitia ofisi ya Rais TAMISEMI  ni kwa sababu serikali inatarajia mabadiliko makubwa ya utendaji kazi wenu katika kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu ili kuharakisha maendeleo katika sekta mbalimbali, kupitia mafunzo haya nendeni mkatekeleze majukumu yenu kwa ubora zaidi, ni matarajio yetu Shinyanga itakuwa ni sehemu ya mfano”, ameongeza Ndalichako.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa serikali za mitaa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Hamisi Mkunga amewataka wakawe walimu kwa wengine ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo yaliyohusu  maadili na majukumu kama viongozi wa ngazi husika

“Leo tunahitimisha Mafunzo haya ya awamu ya pili ya kuwajengea uwezo maafisa tarafa na watendaji kata yaliyohusisha mikoa nane ambayo ni Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Pwani, Dae es salaam, Lindi na Mtwara, kile tulichokipata kupitia mafunzo haya tukawe walimu kwa watu wengine ambao hawakupata nafasi ya kushiriki mafunzo haya lakini pia mafunzo haya yawe chachu ya mabadiliko kwenye majukumu yetu ya kila siku na pia ofisi ya taifa TAMISEMI itahakikisha unawapima kwa kile kilichoelekezwa”, amesema Mkunga.

Nao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Abel Kaholwe na Emmanuel Enock wameishukuru ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutoa mafunzo hayo kwani itaenda kuongeza chachu ya utendaji kazi kwenye maeneo mbalimbali.

“Kwanza tunamshukuru Mheshimiwa Rais kupitia ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kutuletea mafunzo haya yatakayokwenda kuongeza chachu ya utendaji kazi kwenye maeneo yetu na kutukumbusha wajibu wetu kama viongozi pamoja na kuzingatia kanuni na maadili ya kazi yetu”, amesema Emmanuel Enock.
Afisa elimu Mkoa wa Shinyanga Dafroza Ndalichako akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Hamisi Mkunga akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya muda mfupi TPSC Hosea Goerge akitoa mafunzo.
Afisa Mtendaji Kata ya Mwamasa Halmashauri ya Msalala Abel Kaholwe akizungumza mara baada ya mafunzo hayo.
Afisa Mtendaji Kata ya Salawe Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Emmanuel Enock akizungumza baada ya Mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post