Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mbunge wa Nanyamba (CCM), Abdallah Chikota ameshauri serikali itoe vivutio maalum kwa wawekezaji wanaotaka kujenga vituo vya kujazia gesi asilia ili kusogeza huduma kwa wananchi wanaofunga mfumo wa gesi kwenye vyombo vyao vya usafiri.
Akichangia mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2024/25 bungeni, Chikota amesema kwasasa vituo hivyo vipo vinne nchini huku kampuni zaidi ya 30 zikiwa zimeomba.
“Tuwe na vivutio ili kutoka Dar es salaam kuja Dodoma kuwe na vituo vya gesi na maeneo mengine, tutoe punguzo maalum ili wawekezaji wajikite kwenye eneo hili,”amesema.
Kuhusu usambazaji wa gesi viwandani na majumbani, Chikota amesema pamoja na kazi inayofanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) lakini haipewi fedha za kutosha.
“Naomba mpango ujielekeze kutoa fedha za kutosha ili usambazaji huu sasa uende kwenye mikoa yote isiwe Mtwara, Lindi na Dar es salaam,”amesema.
Aidha, amepongeza Wizara ya Nishati kwa kazi inayofanya kwenye gesi asilia huku akishauri shughuli za mradi wa gesi asilia zifanyike kwenye eneo husika.
“Likong’o ipo Manispaa ya Lindi si busara shughuli hizi zikaendelea kufanyika Dar es salaam na Arusha wakati eneo la mradi lipo naomba sasa shughuli za LNG zihamie eneo husika, kuhusu vituo vya kujazia gesi vipo vichache,”amesema.
Kadhalika, Mbunge huyo ameshauri katika sera ya elimu ya mwaka 2014 toleo la 2023, serikali ijielekeze katika ugharamiaji kwa kuwa inakwenda kubadili uendeshaji na usimamizi wa elimu.
“Kuanzia mwakani tunaanza kutekeleza mtaala mpya inamaana mtihani wa darasa la saba 2027 hautakuwepo kutakuwa na mtihani wa tathmini, takwimu zilizopo wanafunzi takribani asilimia 25 hawaendelei na kidato cha kwanza, hivyo tutakavyokuwa tunafanya tathmini wanafunzi wote wataingia kidato cha kwanza,”amesema.
Amesema kutakuwa na mahitaji mapya ikiwamo madarasa, walimu, vyoo na kwamba inakadiriwa kuhitajika madarasa ya ziada 8733, vyoo 17,467 na kusisitiza lazima mpango ujikite katika kutafuta fedha za kugharamia mfumo mpya wa elimu.
Social Plugin