MHANDISI LUHEMEJA AANIKA MAFANIKIO UJENZI WA KIWANDA CHA SUKARI MKULAZI


*Aipongeza NSSF kukamilisha kiwanda hicho ambacho kimeanza uzalishaji

*Asema kitaongeza upatikanaji wa sukari nchini na kutoa ajira kwa Watanzania

Na MWANDISHI WETU

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja, amepongeza kazi kubwa iliyofanywa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ya kujenga kiwanda cha sukari Mkulazi kilichopo Mkoani Morogoro.

Mhandisi Luhemeja alisema hayo leo tarehe 30 Novemba, 2023 wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za NSSF zilizopo katika Jengo la Benjamini William Mkapa, jijini Dar es Salaam na kuzungumza na Menejimenti ya Mfuko huo.

Alisema ujenzi wa kiwanda hicho ambacho kimeanza kufanya kazi ya uzalishaji wa sukari ni hatua kubwa kwa Taifa kwa sababu kitaongeza upatikanaji wa sukari, kitazalisha ajira kwa Watanzania na kitachangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Ujenzi wa kiwanda hiki ni hatua kubwa sana kwa nchi yetu, kwa sababu kitaleta tija kwa NSSF, Taifa na jamii kwa ujumla,” alisema Mhandisi Luhemeja.

Alisema faida nyingine ya kiwanda hicho ni kuwa kimezalisha ajira za moja kwa moja 11,000 jambo ambalo Mfuko umeweza pia kuongeza kiwango cha ajira kwa Watanzania na kwamba katika awamu ya kwanza kitazalisha tani za sukari 50,000 lakini lengo ni kuzalisha tani 75,000.

“Haya ambayo yamefanywa na NSSF katika kiwanda hiki cha sukari ni mapinduzi makubwa sana na ukiangalia sera ya Mfuko inataka tuwekeze kwenye maeneo yenye tija kama haya,” alisema Mhandisi Luhemeja.

Akizungumzia uwekezaji wa majengo, alisema NSSF pia inafanya vizuri kwa kujenga majengo mazuri na yenye viwango, huku akionesha kuvutiwa na uwekezaji wa hoteli ya kitalii yenye hadhi ya nyota tano iliyopo jijini Mwanza.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Luhemeja aliipongeza NSSF kwa kuendelea kufanya vizuri katika kutekeleza majukumu yake ya msingi huku akiiomba Menejimenti kuendelea kuongeza kasi ya kuandikisha wanachama wapya ili kuongeza idadi ya wanachama wachangiaji.

Mhandisi Luhemeja aliwaomba NSSF kushirikiana na taasisi nyingine kama Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ili waweze kuunganisha nguvu ya pamoja kwa lengo la kusajili waajiri na wafanyakazi wengi zaidi.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba alimshukuru Mhandisi Luhemeja kwa ziara hiyo ambapo aliahidi kuwa maagizo na maelekezo yaliyotolewa na Katibu Mkuu huyo watayafanyia kazi hasa katika kuongeza idadi ya wanachama wachangiaji.

Alisema Mfuko unaendelea kuboresha huduma zake kwa kutumia mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kuwarahisishia wanachama na wadau kupata huduma kwa urahisi popote walipo bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post