Na John Mapepele
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki ameongoza kundi maalum la wawekezaji na watalii mahiri duniani zaidi ya 150 kutoka nchini Marekani na nchi nyingine duniani lililowasili nchini Novemba 4, 2023 kucheza Singeli kutoka kwa msanii nguli nchini Sholo Mwamba katika hafla maalum ya kuwaaga wageni hao baada ya kutembelea vivutio mbalimbali.
Hafla hiyo imefanyika jijini Arusha Novemba 12, 2023 na kupambwa na vikundi mbalimbali vya utamaduni ikiwa ni pamoja na Wanne Star na Warriors From the East ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu Mhe, Dotto Biteko aliyewakilishwa na Mhe. Prof, Kitila Mkumbo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji) ikiwa ni mkakati maalum wa Serikali wa kuitangaza Tanzania duniani kimataifa na kusaka soko la kimkakati la Amerika.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyowajumuisha mabilionea na wafanyabiashara wenye makampuni makubwa duniani kama Amazon, na Fueled na wasanii wa Hollywood, Mhe. Kairuki amesema Tanzania imebarikiwa kuwa na mazao mengi ya utalii yenye viwango vya kimataifa ambayo yametapakaa katika kila kona ya nchi yetu kuanzia kaskazini hadi kusini na amewashawishi kuja kutembelea maeneo hayo.
Ameyataja baadhi ya maeneo hayo yenye viwango vya kimataifa kuwa ni pamoja na Mbuga na Hifadhi za Wanyama na fukwe zenye viwango vya kimataifa ambazo hazipatikani katika maeneo mengi duniani.
Amesema sekta ya utalii inachangia taifa zaidi ya bilioni 2.6 za kimarekani na kuzalisha zaidi ya ajira milioni 1.5 ambapo inachangia asilimia 17.2 katika uchumi wa Tanzania.
Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuitangaza Tanzania kupitia Filamu ya The Royal Tour ambayo imesaidia wawekezaji hao kutambua vivutio na kuja kutembelea.
Social Plugin