Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MIUNDOMBINU YA UMEME ITAKAYOENDESHA TRENI YA MWENDO KASI (SGR) KUKAMILIKA JANUARI 2024

 





Leo tarehe 16 Novemba, 2023 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Kilumbe Shaban Ng'enda imetembelea na kukagua miundombinu ya umeme iliyojengwa na TANESCO kwa ajili ya kuendesha treni ya kisasa ya mwendokasi (SGR) pamoja na mitambo ya uzalishaji Umeme wa Gesi Asilia ya Kinyerezi I (MW 150), Kinyerezi II (MW 240) pamoja na Mradi wa Upanuzi wa Kituo cha Kinyerezi (MW 185) iliyopo Dar es Salaam.


Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Shaban Ng'enda, amesema kuwa ziara hiyo ilianza tarehe 11 Novemba, 2023 kwa lengo la kuangalia namna ambavyo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia Wizara ya Nishati limekuwa likitekeleza mradi wa miundombinu ya umeme itakayoendesha treni ya mwendokasi (SGR), wakianza na vituo vya Morogoro na kuhitimisha kituo cha Kinyerezi.


*"Sisi kama Kamati tumeridhishwa na maendeleo ya kazi hii, kwasababu mradi huu kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro umekamilika kwa asilimia 100 na Morogoro hadi Kintiku mkoani Singida kwa asilimia 99.Tumeridhishwa na tunawatia shime wafanyakazi wote wa Wizara ya Nishati na TANESCO kwa ujumla kusimamia kazi hii kwa umakini mpaka itakapokamilika"* Amesema Mhe. Ng'enda


Amesisitiza kuwa, TANESCO kwa kushirikiana na Shirika la Reli Tanzania (TRC ) kuwa na mitambo ya akiba (backup) itakayosaidia endapo kutakuwa na dharula kwenye Grid ya Taifa ili treni ya mwendo kasi iendelee kufanya kazi.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha fedha takribani bilioni 76 ili kufanikisha miundombinu ya umeme kwa ajili ya mradi wa treni ya mwendokasi.


*“Sisi Wizara ya Nishati tumeshirikiana na Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha miradi hii inatekelezwa vizuri na sasa tumekamilisha kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Kingorwila, Morogoro. Tunamshukuru sana Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jwmhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo yake, vile vile kwa kutenga fedha kwa ajili ya miradi hii ambayo ina maslahi kwa maendeleo ya Tanzania. Sisi kama Wizara ya Nishati tukiongozwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Mashaka Biteko tutasimamia miradi hii kwa ufanisi mkubwa na kuhakikisha inakamilika kwa wakati"* Amesema Mhe. Kapinga


Aidha, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, amewashukuru wataalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Wizara ya Nishati kwa kushirikiana pamoja katika kufanikisha utekelezaji wa mradi wa miundombinu ya kuendesha treni ya SGR. Amesema kuwa hadi sasa wanategemea kupokea vichwa vya treni ya mwendo kasi na kufanya majaribio ili kujiridhisha na utendaji kazi wake ambayo itatembea kwa mwendo wa kilomita 160 kwa saa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com