Na John Mapepele
Kamati ya kitaifa ya Kuandaa Mpango Kamambe wa kuendeleza Sekta ya Ufugaji wa Nyuki nchini unaojulikana kama “Achia Shoka Kamata Mzinga” leo Novemba 16,2023 imewasilisha rasimu ya mpango huo kwa wadau wa sekta hiyo baada ya kukamilisha kazi ya kuuandaa na kupata maoni nchi nzima ili uende mbela kwa hatua zaidi.
Mpango huo wa Achia Shoka, Kamata Mzinga umelenga kuweka mazingira wezeshi ya wananchi kunufaika na rasilimali za nyuki na misitu na kuboresha uzalishaji na uuzaji wa asali ndani na nje ya nchi ambapo kwa sasa Tanzania inazalisha tani 32000 wakati uwezo wake ni tani138000 kwa mwaka.
Akifungua warsha hii ambayo imewajumuisha wadau wote kwenye mnyororo wa thamani wa uzalishaji wa asali nchini ya kupokea maoni ya rasimu ya Mpango huo, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo, Dkt. Edward Kohi amesema warsha hiyo imewashirikisha wabobezi wote wa sekta na amewasihi watumie nafasi hiyo kuchangia mawazo yao ili kupata mpango utakaokuwa mwarobaini wa changamoto zinazokabili sekta hiyo kwa sasa.
"Pamoja na uwepo wa mikakati na jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau wa sekta binafsi, bado kiwango cha uzalishaji wa asali na mazao mengine ya nyuki na biashara ya asali hasa katika masoko ya nje ya nchi hakiridhishi hivyo tutumie warsha ya leo kutengeneza kitu ambacho kitakuwa na faida kwa kizazi cha sasa na baadaye kama ambavyo kauli mbiu ya wizara inavyosema kuwa tumerithishwa tuwalithishe” amefafanua Dkt. Kohi
Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuona kuwa mpango huu unaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya ufugaji nyuki na kuongeza mchango wa sekta ya nyuki katika Pato la Taifa
Aidha, amesisitiza kuwa wakati umefika kwa wadau kuangalia namna ambavyo mdudu nyuki anavyoweza kuhifadhiwa vema na kutumika katika utalii wa nyuki ambao ukiendelezwa vizuri utaliingizia taifa.
Pia Dkt. Kohi amewataka wadau wote wa nyuki nchini kujipanga na kuona namna ambavyo wanaweza kunufaika na mkutano mkubwa wa kidunia wa wadau wa nyuki (Apimondia) utakaofanyika nchini 2027.
Makundi yaliyoshiriki warsha hiyo ni kutoka kwenye taasisi na maeneo ambayo shughuli za ufugaji nyuki zimeshamiri, ikijumuisha wafugaji nyuki, wachakataji na wafanyabiashara wa mazao ya nyuki, maafisa ufugaji nyuki wilaya, wadhibiti ubora, watafiti, wanazuoni, wataalamu, wasimamizi na watunga sera.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki ambaye pia ni Katibu wa Kamati hiyo na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Misitu na Nyuki Daniel Pancras aliishukuru Wizara na wadau kwa kuendelea kuweka misingi thabiti ya usimamizi wa raslimali za Misitu na Nyuki na kuandaa mpango huo.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Mkabwa Manoko amemhakikishia mgeni rasmi kuwaanaamini uwezo mkubwa wa wadau utasaidia kutoa maoni yao kwa weledi ili kukiwezesha kamati yake kukamilisha kazi kwa wakati.
Katika kilele cha Siku ya Nyuki Duniani Mei 21,2023 mkoani Singida, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe,Dkt. Philipo I. Mpango aliielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa mpango huo, ndipo wizara ikaunda Kamati Maalum kwa ajili ya kazi hii.`
Social Plugin