Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MKUTANO MKUU WA 28 WA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA USHIRIKA TANZANIA


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

SHIRIKISHO la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) limefanya mkutano wake Mkuu wa  mwaka wenye lengo la kutambua changamoto zinazowakabili katika vyama vya ushirika,tathimini ya mafanikio na suala la kupitia bajeti.

 Akizungumza na waandishi wahabari leo Nov 29,2023 Jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Shirikisho wa Vyama vya Ushirika Tanzania Bw.Charles Jishuli amesema kuwa wameunda tume ya uchunguzi kwa ajili ya kupata taarifa za kutosha dhidi ya vitendo vya unyanyasajj kwa watumishi wa Ushirika, kutokana na malalamiko ya watumishi.

 "Bodi kuna watumishi inaowasimamia na kuna watumishi  wanaopata ajira kupitia bodi na kuna watumishi wanaoajiriwa kupitia menejimenti ya Shirikisho  kuna watumishi kama dereva, karani hawa wameajiriwa na menejimenti ya Shirikisho, haya mambo mnayoyasikia yamekuja baada ya ukaguzi kwamba wakuu wetu wanawafanyia unyanyasaji watumishi". Amesema Bw. Jishuli

Aidha amebainisha kuwa wameunda tume kwa ajili ya kufanya uchunguzi ili kutenda haki kwa watumishi na wanaotuhumiwa kufanya unyanyasaji baada ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusiana na tuhuma hizo.

Pamoja na hayo amesema kuwa ubora wa mazao unahitajika kwa sababu una manufaa na faida katika bei na kupendwa na walaji na unapatikana kuanzia katika uzalishaji, uvunaji na upangaji wa madaraja na uhifadhi katika ghala.

"Katika ubora sisi tuna vyombo vyetu vya ndani kwenye ghala pakuuzia utakuta pale kuna watu wapo wanaoangalia ubora,Ubora ni katika kupanga madaraja na kuangalia unyevu katika mazao ni ule unao hitajika lakini kuna vyombo vingine vya kiserikali vyenye mamlaka vinavyo shughulika katika shughuli za ughani".  Amesema.

Kwa upande wake Makamu mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Ushirika Bi.Sylivia Masawe amesema kuwa mikutano kama hiyo inawapatia fursa kukutana na kutambua changamoto zinazo wakabili na kuzitatua kwa lengo la biashara ili kujikwamua kutoka katika hali ya umaskini kwenda kwenye hali nzuri ya kiuchumi.

"Kwasababu tunaamini ushirika ni chanzo kimoja cha kujikomboa kutoka katika hali  moja ya umaskini kwenda kwenye hali nzuri ya kimaisha, hasa wakati kama huu tunasisitiza kuwa ushirika ni biashara".  Ameeleza.

Naye Mrajisi msaidizi kutoka sehemu ya Sheria na Usajiri Tume ya Maendeleo Tanzania, Bw.Emmanuel Sanka Amesema kuwa wamekutana hapo kwasababu lengo la ushirika ni kujiendesha kidemokrasia na kutimiza takwa la kisheria .

Vile vile Kamishna wa Tume ya Maendeleo nchini  Bw. Godfrey Ng'ura amesema kuwa kwa sasa kumekuwa na muamko mkubwa wa ushiriki kwa kuwa na ongezeko la wanachama wapya na hivyo Shirikisho linahamasisha misingi ya sera,Sheria na utawala bora ili kuwa na vyama bora vya ushirika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com