Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MWAKA MPYA 2024 KUWA NEEMA YA KUWAFAIDISHA MAJISAFI ZAIDI YA WANANCHI ELFU 75.9 WA NZUGUNI


Wananchi wa maeneo ya Nzuguni Jiji Dodoma wameanza kupata huduma ya majisafi kwa majaribio wakati mradi ukiendelea kutekelezwa na ifikapo mwezi Januari, 2024 mradi huo utakamilika kwa asilimia 100.

Mradi huo utakapokamilika utahudumia pia maeneo ya Ilazo,Kisasa nyumba 300 na Swaswa,ambapo kwa sasa umefikia asilimia 96 ya utekelezaji.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule akifanya kazi ya ufuatiliaji wa mradi huo amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Dodoma kuwa changamoto ya uhaba majisafi itaondoshwa ifikapo mwezi Januari, 2024 mradi utakapokamilika, na hilo ndio matumaini makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwaondolea wananchi wake adha ya uhaba wa huduma adhimu ya majisafi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph ambaye ndiye mtekelezaji na msimamizi wa mradi huo amesema ujenzi wa mradi ulianza tarehe 07 Februari , 2023 na utakapokamilika na kuwanufaisha zaidi ya wananchi elfu 75.9 na kufanya ongezeko la asilimia 11 ya hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi kutoka wastani wa asilimia 50 hadi asilimia 61.7 kwa siku.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,Mhe. Alhaj Jabir Shekimweri aliyeambatana na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma katika ziara hiyo ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji -Nzuguni amempongeza Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb), pamoja timu yake yote kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maji mkoani Dodoma, na kwamba kukamilika kwa mradi wa majisafi Nzuguni kutasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza adha ya upatikanaji wa huduma ya majisafi kwa wananchi, pia ameipongeza DUWASA kwa kuanza awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi wa maji kwa kuanza kuchimba visima vitano vya maji.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com