Na Mwandishi Wetu
MWANAMITINDO Jasinta David Makwabe(25) mwenye urefu wa 5’11 Ft ambaye amechaguliwa kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano makubwa ya Future Face 2023 yanayotarajia kufanyika Novemba 25 mwaka huu nchini Nigeria.
Jasinta amechaguliwa baada ya kuibuka mshindi kwa kuwashinda washiriki wengine waliokuwa wakiwania nafasi hiyo ambapo wakati shindano hilo linaanza kulikuwa na washiriki zaidi ya 200 na baada ya kufanyika usahili na kubakia wanamitindo wanne na sasa amepata nafasi hiyo kuiwakilisha nchi kutokana na kukidhi vigezo vinavyotakiwa.
Mashindano ya Future Face kwa nchini Tanzania yamefanyika jijini Dar es Salaam kwa uratibiwa na Mwanamitindo wa kimataifa Millen Happiness Magese aliyeshirikiana na waandaji wa Future Face 2023 duniani.
Majaji ambao ni wabobezi katika masuala ya mitindo na ubunifu wameshiriki katika kuchuja washiriki ili kupata mshindi mmoja mwenye sifa na vigezo vinavyokubalika.
Akizungumza kuhusu mshindi huyo anayewakilisha Tanzania katika mashindano ya Future Face 2023 yaliyofanyika jijini Dar es Salaam , Mwanamitindo wa Kimataifa Millen Happiness Magese amesema Jasinta amechaguliwa baada ya majaji kuangalia sifa na vigezo vya shindano hilo.
Aidha amesema mshindi huyo anatarajia kuondoka nchini usiku wa Novemba 16 kuelekea Nigeria yanakofanyika mashindano hayo ambayo yamekuwa yakifuatiliwa na wanamitindo na watu mashuhuri duniani kote.
"Nawashukuru majaji wote kwa ushiriki na kujitoa kwao kufanikisha jambo hili muhimu ambalo limeandika historia kubwa katika nchi yetu kwani ndio mara ya kwanza Shindano la Future Face kufanyika nchini Tanzania.
" Pia nawashukuru sana vijana wote kwa kujitokeza kwa wingi na hatime tumempata mmoja miongoni mwao kwa ajili ya kwenda kutuwakilisha, amesema Millen wakati akielezea mashindano hayo makubwa duniani ambayo fufanyika kila mwaka.
Pia amevishukuru vyombo vyaa habari nchini ambavyo tangu kuanza kwa usahili ngazi ya wali vimeshiriki kikamilifu na kuripoti kila hatua na hatimaye kupatikana mshindi , hivyo ameedelea kuviomba kuendelea kushirikiana naye katika masuala yanayohusu mitindo na wanamitindo.
Kuhusu shindano hilo, Magese amesema Future Face ni shindano la kipekee lililoandaliwa na Wakala mkubwa zaidi wa wanamitindo barani Afrika Beth Model Management na limekuwa linajivunia utofauti wake wa ukubwa wa kutojali umri, rangi na kabila na kubwa zaidi limejikita katika sera ya fursa sawa.
Kwa upande wake Mwanamitndo Jasinta amesema anamshukuru Mungu kwa kupata nafasi ya kwenda kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Future Face Global yatakayofanyika nchini Nigeria kuanzia Novemba 16 mwaka huu mpaka Novemba 25 ambayo itakuwa fainali.
"Haya mashindano yanahusisha nchi zaidi ya 20 za Afrika , kwa hiyo mimi nimetokea kuwa mwakilishi wa Tanzania , hivyo Watanzania wenzangu naomba maombi yenu , " amesema na kufafanua mshindi atakayepatikana katika mashindano hayo anaweza kuunganishwa kupata kazi katika kampuni kubwa za kimataifa ambazo ziko Paris nchini Ufaransa, New York nchini Marekan na Millan nchini Italia.
Aidha amesema kwake kama binti mwanamitindo ni fursa na bahati kubwa hivyo ameendelea kuwaomba Watanzania wote kuendelea kumuombea ili aweze kushinda ili aiwakilishe nchi yake vema sambamba na kutimiza ndoto zake kama binti wake wa kitanzania.
Social Plugin