Na Mwandishi Maalum, Dar Es Salaam
Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri kuhusu utekelezaji wa ahadi za Nchi kwenye Jukwaa la Kizazi chenye usawa ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amezitaka nchi za kiafrika kuhakikisha zinawekeza ipasavyo na kuweka nguvu kubwa kwenye utatuzi wa changamoto za usawa wa kijinsia.
Ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa neno la shukrani katika Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Mawaziri wa Masuala ya Jinsia kutoka Nchi za Afrika unaoendelea jijini Dar es Salaam.
Amesema ukosefu wa usawa wa kijinsia bado ni changamoto inayoendelea Barani Afrika hivyo, nchi za Kiafrika zinatakiwa kufanyia kazi changamoto hizo ili kuwa na dunia na Bara lenye haki na usawa kwa wanawake na wasichana wote.
“Ni lazima tuwekeze katika elimu, huduma za afya, uwezeshaji wanawake na wasichana kiuchumi lakini pia afua zingine na kuongeza usikivu ili kushughulikia mila, desturi na fikra potofu ambazo zinawarudisha nyuma wanawake” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Ameongeza kuwa nchi za Afrika zinatakiwa kuwa na ubunifu katika kutafuta ufadhili wa masuala ya usawa wa kijinsia kama vile Serikali kuingia ubia na Sekta Binafsi na pia kuchangia kupitia bajeti za Serikali.
Aidha, Mhe. Kairuki amezitaka nchi za Afrika kuongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya programu za usawa wa kijinsia na kuhakikisha zinatumika ipasavyo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kairuki amewaalika washiriki wa mkutano huo kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyoko nchini ikiwemo utalii wa kihistoria, utamaduni, wanyamapori na vinginevyo.
Social Plugin