Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NEMC YAPONGEZWA KUHAKIKISHA INASHIRIKIANA NA WANANCHI KWENYE UTUNZAJI WA MAZINGIRA


NA EMMANUEL MBATILO, MKURANGA

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeipongeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kuendelea kushirikiana vizuri na wenye viwanda pamoja na wananchi kwa ujumla katika suala zima la utunzaji wa mazingira.

Pongezi hizo zimetolewa leo Novemba 13,2023 Mkuranga mkoani Pwani na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Anna Lupembe walipofanya ziara ya kutembelea kiwanda cha Lodhia ambapo wameridhishwa na suala la utunzaji wa mazingira kwenye kiwanda hicho.

Amesema kuwa awali kiwanda hicho kilikua hakijafuata taratibu za kimazingira hivyo ametoa wito kwa wamiliki wengine wa viwanda kufanya marekebisho sehemu ambazo zinakiuka taratibu za kimazingira.

“Kiwanda hiki kilikuwa kikitoa moshi sana, sasa hivi moshi sio kero kwa Wananchi, tunapenda mazingira ya viwanda yawe rafiki na jamii, baada ya Waziri Jafo kutoa maelekezo yamezingatiwa na kufanyiwa kazi, nawapongeza sana". Amesema

Aidha Mhe. Lupembe amesema kuwa Serikali inawakaribisha wawekezaji kuwekeza katika Viwanda Jambo ambalo litachangia kuajiri vijana wengi nchini wanaohitimu katika mafunzo ya ufundi yanayosimamiwa na taasisi mbalimbali.

"Kutokana na sera za nchi yetu tunahitaji sana wawekezaji kwenye viwanda ili waweze kuajiri vijana wetu kutoka vyuo mbalimbali, tunaona Rais amewekeza sana katika vyuo vya VETA, kwahiyo tutaendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha wawekezaji". Amesema

Pamoja na hayo amepongeza Rais Samia kwa kufungua fursa ya uwekezaji nchini ambapo imechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa bidhaa nchini ambazo zamani ilikua zinaagizwa kutoka nje ya nchi kwa gharama kubwa.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Saidi Jafo amesema lengo la ziara hiyo ni kuendelea kufanya uhakiki ili kuona maendeleo mbalimbali yanayozingatia matakwa ya utunzaji wa mazingira.

Hata hivyo Waziri Jafo amewataka wawekezaji wengine kufuata taratibu za kimazingira ili kuepusha kufanya uchafuzi ambapo itapelekea ongezeko la joto.

"Moshi ukitiririka inasababisha ongezeko la joto unajua kutokana na mkataba wa Paris unasema joto linatakiwa lisifike nyuzi joto 2°". Ameeleza Dkt. Jafo.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa kiwanda Cha Lodhia Bw.Saleish Pandit ameishukuru kamati hiyo kutembelea katika kiwanda chao ambapo itawasaidia wao kuendelea kufanya maboresho na kuchangia katika sekta ya ajira na kodi kwaajili ya kukuza uchumi wa nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com