Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PROF.ABDULRAZAK GURNAH MGENI RASMI TUZO YA TAIFA YA UANDISHI BUNIFU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 24,2023 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ambayo inatarajiwa kufanyika February 13,2024 ambayo ni siku ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

***************

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MWANDISHI Mkongwe wa Machapisho Prof.Abdulrazak Gurnah anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika utoaji Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ambayo itafanyika February 13,2024 ambayo ni siku ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 24,2023 Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa wameongeza vipengele vya shindani ambapo kuna riwaya,ushahiri,na hadithi za watoto, tofauti na mwaka uliopita ushindani ulikuwa kwa nyanja mbili tu ambazo ni Riwaya na Ushahiri.

"Tunawajibu wa kukuza Uandishi Bunifu ambao unakuza maadili yetu na uzalendo kwa nchi yetu, lengo la tuzo hizi ni kuwatambua waandishi mahiri na malengo mengine ni kukuza lugha ya Kiswahili, kukuza utamaduni wa kujisomea , kuhifadhi historia na mitizamo bora ya Taifa la Tanzania". Amesema

Aidha amewataka waandishi bunifu kuwasilisha miswada yao kwa wakati kwani muda uliobaki ni mchache, hivyo wanatakiwa kuwasilisha mapema huku wakizingatia utaratibu ambao umewekwa na wahusika.

"Mpaka sasa muitikio ni mzuri sana kwa washiriki ambapo tulitangaza mwisho wa kupokea miswada ni Novemba 30,2023 kwahiyo natumia fursa hii kuwaambia waandishi bunifu kuwasilisha miswada yao kwa utaratibu uliowekwa". Amesema Prof. Mkenda.

Prof. Mkenda amesema wanatarajia kutoa tuzo kwa Mshindi wa kwanza hadi watatu, na zawadi za tuzo hizo ni Shilingi Milioni kumi kwa mshindi wa kwanza ambaye atapata pia ngao ya ushindi na andiko lake litahaririwa na kuchapishwa na Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na kuvigawa katika maktaba mbalimbali nchini.

Amesema mshindi wa pili atapokea Shilingi Milioni saba na cheti, mshindi wa tatu atapokea Milioni tano na cheti na washiriki wengine watakao bahatika kushika nafasi ya nne hadi kumi watatajwa na watapewa vyeti vya pongezi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hizo, Prof. Penina Mlama amesema kuwa tuzo wanazozitarajia kuzitoa zinazingatia kanuni na taratibu ambazo walipewa washiriki kuanzia idadi ya maneno katika miswada yao na muda wa kuwasilisha miswada .

"Tuliweka vigezo maalumu ambavyo waandishi hawa wanapaswa kufuata, kuna vigezo vya urefu mfano kwa upande wa riwaya tunategemea maneno Elfu sitini (60,000) na yasiyozidi laki moja (100,000), na kwa upande wa ushahiri tunategemea mashahiri yasiyozidi 60. Kwa upande wa Vitabu vya watoto ambapo kwa mara ya kwanza tumeingiza kwenye mashindano, mara nyingi Vitabu vya watoto havina maneno mengi zaidi ya picha, tunategemea maneno yasiyozidi Elfu moja". Ameeleza Prof .Mlama

Pamoja na hayo amesema kila nyanja ina majaji watatu waliobobea katika masuala ya Uandishi Bunifu na baada ya kukusanywa miswada hiyo majaji wataisoma kwa miezi minne ndipo baada ya miezi hiyo itafuatia hafla ya utoaji wa tuzo hizo.

Vilevile Prof. Mlama amewashukuru waandishi wa habari kwa kushiriki kutangaza tuzo hizo kwa mwaka uliopita ambapo walifanikiwa kuzipa uzito mkubwa na kutambulika ndani na nje ya nchi.

"Naomba niwashukuru sana waandishi wa habari, tuzo hii iliweza kufahamika Tanzania na nje ya Tanzania kutokana na kazi nzuri waliyoifanya waandishi wa habari, tunawashukuru sana". Amesema
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Carolyne Nombo akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 24,2023 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ambayo inatarajiwa kufanyika February 13,2024 ambayo ni siku ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, Prof. Penina Mlama akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 24,2023 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa kuhusu Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ambayo inatarajiwa kufanyika February 13,2024 ambayo ni siku ya kuzaliwa kwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com