Na Dotto Kwilasa,Dodoma
WADAU wa afya nchini wametakiwa kuendeleza mapambano dhidi ya tatizo la usugu wa vimelea vya dawa kwa kuongeza uelewa kwenye jamii na kutia hamasa kuhusu usugu wa dawa za binadamu ambao unatishia afya za binadamu duniani kote.
Hayo yamelezwa hivi karibuni jijini hapa na Mkurugenzi wa huduma za dawa na Mfamasia Mkuu wa Serikali Daud Msasi wakati wa maashimisho ya wiki ya kuongeza uelewa wa usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa ambayo iliambatana na matembezi ya kuhamasisha jamii kuachana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa.
Aidha matembezi hayo yaliyoratibiwa na Shirika lisilo la kiserikali linalojikita kupambana na usugu wa vimelea vya dawa (RBA-INITIATIVE)yanatajwa kujenga na kuongeza uelewa kwa wananchi na wafamasia kwa ujumla kuwa na utaratibu wa kutoa huduma baada ya kupokea cheti kutoka kwa Daktari ili kunusuru afya za watu.
Amesema wananchi wanapaswa kuzingatia matumizi ya dawa aina ya Antibiotics kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa afya na kwamba Serikali inapambana kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na afya njema bila ili shughuli za kijamii ziende sawa.
"Katika zama hizi bado kuna baadhi ya watoa huduma za afya nchini hawazingatii taratibu za kitabibu katika kutibu wagonjwa kwa kuwapatia dawa bila utaratibu maalumu, niwaombe kila mtu azingatie matumizi sahihi ya dawa," ameeleza.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mradi (RBA-INITIATIVE) Michael Mosha amesema kuwa wameanza na kampeni hiyo kwa kuwashirikisha wadau wa elimu na wasanii kwa lengo LA kuifikia jamii na kuwa na jamii salama yenye afya njema.
Amesema ni mumuhimu elimu zaidi kutolewa kwa jamii ili kuongeza uelewa kuhusu usugu wa dawa za binadamu unaotokana na utolewaji wa dawa kiholela bila cheti cha daktari na kusababisha madhara kwa afya ya binadamu.
Aidha amebainisha baadhi ya sababu zinazochangia usugu wa dawa kwa binadamu kuwa ni pamoja na kutumia dawa bila kupima na kupata ushauri wa kitabibu,kutokukamilisha dozi pamoja na matumizi ya dawa za binadamu kwa mifugo .
Aidha amesema wao kama wadau wa kupambana na tatizo la usugu wa vimelea vinavyosababishwa na matumizi mabaya ya dawa wanaanda mpango mkakati ambao Utasaidia kutokomeza usugu wa dawa ili kulinda maslahi ya watanzania kwa ujumla.
"Kwa kuzingatia umuhimu wa afya ya watanzania shirika let linafafanya kampeni ya kukomesha usugu wa dawa kwa jamii yenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu usugu wa dawa za binadamu,tunajikita zaidi kutoa elimu kwa jamii namna ya kuepukana na tatizo la usugu wa dawa kwa kusisitiza zaidi matumizi sahihi ya dawa yanayotolewa na wataalamu ambapo kwa kuanza tayari kumezifikia shule za msingi hadi vyuo vikuu kwani tunaamini ni mabalozi wazuri,”amesema
Nao baadhi ya wanafunzi wa Kata ya Bahi wanaoguswa na kampeni hiyo ya kutokomeza usugu wa vimelea vya dawa wameiomba mamlaka ya usimaminzi wa chakula na dawa (TMDA) kuhakikisha wanayafungia maduka yote ya dawa ambayo yanaendelea kukiuka taratibu za kifamasia .
Jesca John mwanafunzi wa shule ya Msingi Bahi-Dodoma ameeleza kuwa iwapo maduka ya dawa yatadhibitiwa hali ya afya kwa binadamu itakuwa salama na kwamba lazima sheria na miongozo ya kiafya ifuatwe na wafamasia kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia utekelezaji wa sheria za afya.
"Usugu wa dawa ni hali ya dawa kushindwa kuua vimelea vya magonjwa au kuzuia ukuaji wake na hivyo dawa kushindwa kudhibiti vimelea hivyo,napenda kuikumbusha jamii kuwa vimelea vya magonjwa ndio hujenga usugu wa dawa,jamii na hasa sisi wanafunzi tunapaswa kupiga Vita matumizi mabaya ya dawa,"amesema.
Social Plugin