Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Lugano Kusiluka. |
Na Dotto Kwilasa, Dodoma
SERIKALI imesema itashirikiana na Wataalam walioko vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu katika kufanikisha tafiti zao kwa kutenga fedha inayokidhi ili kuongeza ubora kwenye kada hiyo
Hayo yameelezwa na Waziri wa Madini nchini Anthony Mavunde katika kongamano la 14 la kitaaluma lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)ambapo ameeleza kuwa kwa kufanya utafiti kwa kina itasaidia kutatua changamoto katika jamii na kuiwezesha Tanzania kupiga hatua.
Amesema maendeleo yanategemea utafiti unaweza kusaidia kujibu changamoto zilizopo kwenye jamii na kuonyesha mwelekeo wa nchi.
“Nitumie fursa hii kuzitaka taasisi za elimu ya juu, kuwa sehemu ya mafanikio ya Tanzania kupitia utafiti ambao unalenga kuifanya nchi yetu kuwa bora zaidi duniani na kupiga hatua katika nyanja za kiuchumi na kijamii.”
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Lugano Kusiluka, ameeleza kuwa katika kutekeleza azma ya kuiwezesha Tanzania kupiga hatua za maendeleo ni lazima wasomi wakubali kishirikiana na taasisi za elimu ya juu hasa upande wa utafiti.
Amesema wao wakiwa wadau wa masuala ya utafiti wameweka mikakati mbalimbali ikiwemo kusimamia ubora wa taaluma inayotolewa na kwamba Chuo chochote duniani, mtaji
wake mkubwa ni wanafunzi waliomaliza katika vyuo husika .
"Tumewakutanisha wahitimu kwa lengo la kujadiliana mambo mbalimbali yatakayoleta maendeleo,UDOM tunayoitaka tunataka iwe iliyoendelea ambayo itakuwa haina shida ya maji, mlipuko wa magonjwa, maabara za kisasa na kutoa taaluma ambayo itawafanya wahitimu wanapohitimu waendane na mahitaji ya soko la ajira kitaifa na kimataifa,” amesema.
Naye Rais wa serikali ya wanafunzi UDOM kwa mwaka 2022/2023, Tryphone Mwinuka, ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa wapo mbioni kuifikia UDOM wanayoitaka kwa kuangalia namna wanavyoweza kuruhusu wanafunzi kufanya biashara kujijengea uzoefu wa kujitegemea na kufafanua kuwa sheria za chuo zinazuia wanafunzi kufanya biashara wanapokuwa katika mazingira ya chuo, jambo ambalo linasababisha kukosa uzoefu wa ujasiriamali wanapohitimu masomo katika taaluma mbalimbali.
"Uongozi wa chuo uangalie namna ya kuiondoa sheria inayozuia wanafunzi kufanya biashara wanapokuwa katika mazingira ya chuo, hali hii inasababisha wanafunzi wengi kukosa uzoefu wanapomaliza chuo, hivyo kushindwa kujiajiri,” amesema.
Mwanafunzi Crispo Vicent, ameuomba uongozi wa chuo kuwaangalia watu ambao wanawasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa kuwapa motisha ili kuwawezesha kuwa na ari ya usaidizi.
"Chuo kitambue kuwa watu wenye ulemavu hata chakula hawawezi kupata bila usaidizi, hivyo tunaomba Chuo kuwajali wasaidizi wetu kwa kuwapatia wasaidizi chochote , kuna wakati wanafanya kwenye mazingira magumu sana," amesema
Social Plugin