Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAKUKURU YAWATAKA WATUMISHI WA UMMA KUTOJIHUSISHA NA VITENDO VYA RUSHWA,UBADHIRIFU


Na Mwandishi Wetu,Kongwa-Dodoma

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilayani Kongwa Dodoma imewataka watumishi wa umma kutojihusisha na vitendo vya Rushwa ili waweze kuihudumia Jamii kwa misingi ya usawa.

Kauli hiyo imetolewa na Maafisa wa TAKUKURU wakati wakitoa Elimu ya Rushwa na athari zake Kwa watumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Kongwa.

Mkuu wa TAKUKURU Wilayani Kongwa  Cosmas Shauri ametumia fursa ya kikao hicho kufafanua Mazingira na tafsiri ya Rushwa katika shughuli za Serikali huku akisisitiza athari za Rushwa kwenye Sekta ya Afya ikilinganishwa na Sekta nyinginezo.

Ametolea mfano kuwa baadhi ya Wananchi wamekuwa wakilazimika kutoa Rushwa Ili kunusuru maisha ya ndugu zao huku wakitambua kuwa kufanya hivyo ni kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa.

Kwa upande wake  Hamad Kibwana Afisa wa TAKUKURU Kongwa amesisitiza watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni za Utumishi wa umma ili kujiepusha na athari za Rushwa katika  Utumishi wao, na kwamba TAKUKURU haitosita kumchukulia hatua Mtumishi yeyote atakayebainika na ukiukwaji wa makusudi wa sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa.

Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Dkt. Majaliwa amehoji Taasisi hiyo ikiwa ni halali kwa wagonjwa kuwapelekea zawadi watumishi kwa madai ya kuridhishwa na huduma zitolewazo, jambo ambalo Maafisa wa TAKUKURU walilitolea ufafanuzi. wakifafanua hoja hiyo walisema utaratibu wa utoaji na upokeaji wa zawadi kwenye Utumishi wa umma unapaswa kuzingatiwa ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa msimamizi wa kazi (Mwajiri) Ilimaamuzi kuhusu matumizi ya zawadi hiyo yafanyike.

Nao baadhi ya Watumishi hao wakiwemo Remija  Ng'ingo na Maneno Chamgeni wameishukuru TAKUKURU kwa kuwatembelea na kuwakumbusha wajibu wao kiutumishi, na wameiomba Taasisi hiyo kufika mara kwa mara kuwakumbusha na kuwapa Elimu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com