SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa Elimu kwa umma kuhusu masuala ya Viwango katika ngazi za wilaya ambao elimu hiyo imetolewa katika Halmashauri za wilaya za Masasi , Nanyumbu, Newala, Tandahimba na Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara.
Akizungumza wakati wa Kampeni hiyo, Afisa Masoko TBS Bw. Mussa Luhombero amesema lengo la Shirika hilo ni kutoa Elimu Kwa Umma kuhusu umuhimu wa kusoma taarifa zilizopo katika bidhaa, kununua bidhaa zilizothibitishwa ubora wake sambamba na kuwahamasisha wajasiriamali wadogo kuthibitisha ubora wa bidhaa zao na wafanyabiashara kusajili maduka ya chakula na vipodozi.
Kampeni hiyo ya Elimu kwa umma imefanyika katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Sokoni, Stendi, Minadani na maeneo mengine ya wazi ambapo wananchi walijitokeza kupata elimu na ufahamu wa masuala mbalimbali yahusuyo Ubora wa Bidhaa.
Kwa upande wake Afisa Usalama wa Chakula Mwandamizi (TBS) Bw. Barnabas Paul amewasisitiza wajasiriamali na wafanyabishara kuhakikisha wanauza bidhaa zilizothibitishwa ubora wake na TBS na wenye majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi kuyasajili ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Barnabas aliwafafanulia wananchi umuhimu wa viwango katika maisha yao ya kila siku na kuwaasa wawe mabalozi wa kuhamasisha ubora katika jamii wanazoishi sambamba na kutoa taarifa katika ofisi ya TBS zilizopo karibu au kupiga katika kituo cha huduma kupitia mawasiliano yaliyotolewa iwapo watakutana na changamoto zihusuyo masuala ya ubora wa bidhaa wakati wa manunuzi.
Wananchi wamelipongeza Shirika la Viwango Tanzania Kwa kutoa Elimu hiyo kwani itawasaidia kufanya maamuzi sahihi wakati wa kununua bidhaa.
Kampeni hii imeweza kuwafikia wananchi 6220 kati yao wajasiriamali ni 158 na wananchi 6062