Na Dotto Kwilasa,Dodoma
BAADHI ya wananchi Mtaa wa Chimalaa na Ntyuka Jijini hapa wameiomba Serikali kuwashughulikia Watendaji wake wa ngazi ya Kata wanaoshindwa kuiwakilisha vyema kupitia utatuzi wa kero za wananchi ili kupunguza Migogoro isiyokuwa na tija inayokwamisha maendeleo.
Wananchi hao wameeleza hayo leo November 21,2023 Jijini hapa wakati wakizungumza na waandishi wa habari kufuatia kushamiri kwa kero ya Migogoro ya ardhi mkoani hapa jambo linaloelezwa kuwa linachangiwa kwa kiasi kikubwa na viongozi hao wa Kata na Mitaa.
Hatua hii imekuja kufuatia zaidi ya Wananchi 152 wa Mitaa hiyo Jijini kulalamikia Wakala wa Barabara nchini (TANROAD )Mkoa wa Dodoma kwa kutolipwa fidia baada ya kupisha ujenzi wa Barabara licha ya Wakala huo,kuwafanyia uthamini tangu Mwaka Jana na kuahidi kuwalipa fidia ifikapo mwezi juni Mwaka huu.
Aidha Wananchi wa Mitaa hiyo miwili ya Chimalaa na Ntyuka wamepisha ujenzi wa Barabara ambayo inaanzia Kata ya Ntyuka kuelekea Kata ya Kikombo Jijini Dodoma,yenye urefu wa jumla ya Kilomita 76.
Lightness Nkya ameeleza kuwa kero nyingi na Migogoro ya ardhi imekuwa haifafanuliwi vizuri kwa wananchi wa pembezoni na kusabisha Migogoro isiyoisha huku lawama nyingi ikitupiwa Serikali.
"Huenda kero hizi zisingekuwepo kama Watendaji wa Kata wangekuwa wanatupa maelezo ya madai,lakini mara nyingi hawapendi kabisa kutushirikisha na badala yake hutuona wabaya wao pale tunapohoji, " Amesema
Amesema,"Mfano mzuri ni huyu Mtendaji Kata wa Ntyuka hataki kabisa ushirikiano na sisi,lakini angekuwa anatuelewesha tungetulia, wananchi wanataka kueleimishwa tu hakuna asiyetaka maendeleo,tunatambua ili maendeleo yawepo lazima tupishe baadhi ya maeneo, "amesema na kuongeza;
" Inawezekana kabisa labda suala hili lisingefikia hapa kama angetupa ushirikiano, hata tukimuuliza mambo yanavyoendelea huwa anakataa na kutueleza kuwa yeye siyo mhusika," Amesema
Naye Joab Mjilima ameeleza ameshuhudia Mitaa mingi Jijini hapa kuna Migogoro inayozalishwa na baadhi ya viongozi na hivyo kuishauri Serikali kuona haja ya kuingilia kati suala hili ili wananchi waishi kwa amani na kufanya shughuli zao bila kuingiliwa.
"Naamini kabisa watu wengi wamekuwa wakilalamikia Serikali kwa mambo mengi bila kujua watendaji wake wa chini ndiyo wanaoiangusha, tunaomba Serikali iangalie hili watu ambao imewaamini kuwa ni wawakikishi wake huku chini hawatusaidii sisi wanyonge, " Amesisitiza
Kwa upande wa Mwenyekiti wa kamati ya ufuatiliaji wa malipo ya fidia Athanas Matonya ameeleza kuwa mbali na madai hayo yapo madai mengi ambayo wananchi hao wanadai fidia kwa muda mrefu bila kulipwa.
Amesema, "Wananchi wanadai fidia kwenye eneo la Udoma na Chuo cha mwalimu Nyerere ambapo maeneo yamechukukiwa bila kulipwa, tunashangaa wenzetu wa Iyumbu na Nghonghonha wamelipwa lakini sisi hatujalipwa, " Amesema
Mbali na hayo amesema Mradi huo ambao ulianza mwezi Agosti Mwaka 2022 ulipaswa kuanza baada ya malipo ya fidia yao na kwamba serikali inapaswa iwaelekeze nini cha kufanya na ikiwa haiwezekani kuwalipa basi wananchi waelezwe bila fuwaficha.
Naye Michael Tengo ameeleza kuwa kabla ya ujenzi wa Barabara hiyo kuanza, waliahidiwa na wakala huo kulipwa fidia kabla ya ujenzi jambo ambalo halija tekelezwa hadi sasa.
"Tunaomba Rais wetu mpendwa atusaidie hili,Shughuli zetu za uzalishaji zimesimama kwa muda mrefu na hatujui hatma yetu, na juzi walikuja kutuambia tunapaswa kubomoa nyumba zetu kwa hiari hili jambo linatuumiza sana," Amesema
Akizungumzia kuhusiana na suala hilo,Diwani wa Kata ya Ntyuka,Yona Endrew amesema amefuatilia suala hilo kwa Wakala wa Barabara Mkoa wa Dodoma(TANROAD)ambao umekuwa ukitoa ahadi ya kuwalipa wananchi hao lakini haujatekeleza.
Ameeleza kuwa Wananchi hao kwa sasa hawajui ni lini watapata stahiki zao na kubaki na sintofahamu kutokana na Ujenzi huo wa Barabara kuendelea bila wao kujulishwa lolote na hivyo kudhani kuwa huenda wamezulumiwa haki yao.
"Wananchi hawa unaowaona hapo ni katika wana kilio cha muda mrefu takribani Mwaka mmoja Sasa tangu waahidiwe kulipwa fidia kutokana na kusimamisha shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo baada ya maeneo yao kuchukuliwa na Serikali,hivi Sasa wanadai kuambiwa waondoke na wengine kubomoa Nyumba zao bila ya kujua hatima yao, "amesema.
Naye Mhandisi toka Wakala wa Barabara Mkoa wa Dodoma( TANROAD)Calman Gaston,akizungumza na Wananchi hao,kwa niaba ya Meneja wa Wakala huo Mkoa wa Dodoma,amewaahidi wananchi hao kuwa wavumilivu kwani watalipwa stahili zao jambo ambalo liliwafanya wananchi hao kukataa kauli hiyo na kusema kuwa ni uongo kutokana na ahadi hizo kutokewa kila siku bila utekelezaji na kugoma kuondoka katika Ofisi za Kata ya Ntyuka wakishinikiza Meneja wa TANROAD aende kuwalipa fidia zao.
Hata hivyo juhudi za Meneja huyo wa TANROAD kufika katika eneo hilo bado hazikufanikiwa kutokana na kueleza kuwa bado anaendelea na majukumu mengine ya Kiserikali.