WATAFITI WATAKIWA KUFANYA TAFITI ZENYE TIJA

 

 


Wito umetolewa kwa watafiti na wanataaluma nchini kujikita katika kufanya tafiti zenye tija  kwa Taifa  na zinazoleta majawabu kwenye changamoto  zinazoikabili jamii inayowazunguka.

Wito huo umetolewa leo na Naibu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam, Prof. Epaphra Manamba; alipomwakilisha Mkuu wa Chuo katika ufunguzi wa Kongamano la Kitaaluma la Vitivo linalowahusisha wanataaluma na wanafunzi wa shahada ya Uzamili IAA katika kuwasilisha tafiti zao, machapisho na kufanya mijadala ya kina.

 Prof. Manamba amesema kupitia kongamano hilo wanafunzi wamewasilisha tafiti zinazolenga kuangalia Taifa kwa baadaye kwenye maeneo ya Uchumi,Bima,Utalii, Fedha, TEHAMA. Uongozi, Biashara na maeneo mengine, ili jamii iweze kuzipokea na  kutatua matatizo yanayowakabili kulingana na matokeo ya tafiti husika.

“Ni takwa la IAA kila mwanafunzi anayesoma shahada ya uzamili  kufanya utafiti  na kuwasilisha au kuwa na chapisho katika majarida ya kitaifa na Kimataifa,jamii yetu inawategemea hawa watafiti katika utatuzi wa changamoto za kiuchumi na kijamii” alisema Prof. Manamba.

Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti na Machapisho, Dkt. Mordecai Matto amesema zaidi ya tafiti 600 katika maeneo tofauti zimewasilishwa, huku akibainisha kwamba endapo matokeo ya tafiti hizo yatafanyiwa kazi na wadau yatasaidia katika uboreshaji wa sera, na usimamizi na uendeshaji wa taasisi mbalimbali.

Amidi wa Kitivo cha TEHAMA IAA, Prof. Edson Lubua amesema,” wanaofanya tafiti wajikite kwenye changamoto za Watanzania, malengo ya Kitaifa na malengo ya Umoja wa Mataifa, wakijikita hapo watakuwa wamemgusa Mtanzania mmoja mmoja na dunia kwa ujumla”.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Dkt. Suleiman Serera  mwanafunzi wa shahada ya uzamili IAA, ametoa wito kwa wanafunzi wenzake kutoishia kutumia tafiti zao kwa ajili ya kuhitimu na kuzitunza maktaba, badala yake wazitumie kwenye maeneo ya kazi na shughuli zao za kila siku ili kushirikisha jamii kutatua changamoto zao.

Kongamano hili la siku mbili linafanyika moja kwa moja  katika Kampasi za Arusha na Dar es Salaam, walio nje ya Kampasi hizo wanashiriki  kwa njia ya mtandao.












Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post