Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATAKWIMU WATAKIWA KUTOA TAKWIMU SAHIHI KWA VIONGOZI WAO

 
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa akisalimiana na Mkuu wa Miss wa Dodoma Rosemary Senyamule wakati wa hafla ya maadhimisho ya 33 ya kilele cha siku ya Takwimu Afrika 2023 iliyoandaliwa na Ofisi ya Takwimu Tanzania (NBS)

Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa akizungumza kwenye hafla ya maadhimisho ya 33 ya kilele cha siku ya Takwimu Afrika leo November 21,2023 jijini Dodoma. 

Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Watakwimu wa Halmashauri, Wizara, Idara naTaasisi za umma wametakiwa kufanya kazi ya ziada kwa kuwapatia viongozi wao takwimu sahihi ambazo zimepata kibali kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu (NBS)pale wanapowasilisha taarifa kwa wananchi au viongozi wa juu ili kuepuka upotoshaji wa takwimu.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 21, 2023 na Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa wakati wa hafla ya maadhimisho ya 33 ya kilele cha siku ya Takwimu Afrika 2023 yaliyoandaliwa na Ofisi ya Takwimu Tanzania (NBS) ikishirikiana na Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika. ambapo hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya ofisi za Takwimu zilizopo Jijini Dodoma huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule.

Amesema,"Watakwimu, tufanye kazi ya ziada kwa kuwapatia viongozi wetu Takwimu sahihi kwani wanaposimama mbele ya wananchi haipendezi kusikia kiongozi anataka Takwimu ambazo sio sahihi. Tuhakikishe Takwimu tunazowapatia viongozi wetu zimepata Baraka kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu kwani pale ndipo unapata Takwimu sahihi unazoweza kuzitumia sehemu yoyote," Amesisitiza Dkt. Chuwa 

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Rosemary Senyamule amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotoa Takwimu bora ulimwenguni na kwamba umuhimu wa Takwimu kwa nchi za Afrika unaendelea kuboresha hali ya kiuchumi kwa wananchi.

Senyamule amesema Tanzania inatoa Takwimu bora zinazoaminika Afrika na Duniani kwa ujumla na kufafanua kuwa mwaka 2010 Serikali ilitekeleza mradi wa Mpango kabambe wa Takwimu uliotekelezwa hadi mwaka 2018 na ambao uliimarisha upatikanaji wa Takwimu bora nchini. 

"Nitoe Wito kwa Ofisi ya Mtakwimu msambaze taarifa kwenye Halmashauri zetu kwani Takwimu zinatakiwa kutumiwa kwenye kutafsiri mipango ya maendeleo kwa sekta zote. Takwimu zinasaidia nchi za Afrika kufahamu idadi ya rasilimali watu iliyopo na makundi yake," amesema

Naye Kamisaa wa  Sensa kwa upande wa Zanzibar Balozi Mohamed Ally Hamza ameeleza kuwa maadhimisho hayo yana lengo kuu la kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu matumizi ya sensa pia ushirikishwaji wa jamii unasaidia kuongeza thamani ya Takwimu zetu. 

Maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika hufanyika Novemba 21 kila mwaka yakiwa na lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya Takwimu katika mipango ya nchi za Afrika kwani Takwimu zinahitajika wakati wowote.

Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu isemayo "Uboreshaji wa mifumo ya ushirikiano wa kitakwimu ili kuharakisha utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA): Mchango wa Takwimu Rasmi katika mageuzi ya kiuchumi na maendeleo endelevu ya Afrika".

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com