Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATUMISHI UDOM WAASWA KULINDA MAADILI YA UTUMISHI WA UMMA



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Watumishi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wameaswa  kufuata na kuziishi Kanuni na Maadili ya Utumishi wa Umma ili kuwa na Utumishi wa Umma  wenye ufanisi na wa kuheshimika.

Hayo yamesemwa leo  20 Novemba 2023 na mwakilishi wa Kamishna wa Maadili kutoka Ofisi ya Rais - Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kilasara Salvatory alipokuwa akizungumza kwenye semina ya kukuza maadili na kupambana na rushwa mahala pa kazi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza, Jengo la Benjamin Mkapa chuoni hapo.

Amesema watumishi hao wanapaswa kuishi kwa namna ambayo haitoaibisha utumishi wa umma lakini pia kulinda heshima na taswira ya mahala wanapofanyia kazi kwa nia ya kujenga taswira nzuri ya taasisi na utumishi wa umma.

“Mtumishi wa umma, hasa wa Chuo Kikuu, anapaswa kuyaishi maadili ya utumishi wa umma, na kuepuka kusababisha kuongelewa vibaya taasisi anayofanyia kazi” Ameongeza  Kilasara.

Naye mwakilishi wa Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Dodoma Faustine Malesha amewaonya watumishi hao kutoka Kurugenzi na Idara za  UDOM  kuepuka vitendo vya  rushwa na utovu wa maadili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku na kuwaasa kuepuka matumizi yanayozidi kipato kwani yanapelekea vishawishi vya kuomba na kupokea rushwa.

“Nawasihi kutekeleza majukumu yenu ya kila siku kwa weledi na uadilifu ili kuepukana na vitendo vya rushwa kwenye eneo lenu la kazi” amesema

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya kudhibiti uadilifu UDOM, Dkt. Ombeni Msuya amesema kuwa, mtumishi yeyote wa UDOM ambaye ameshindwa kuwa mtendaji mzuri na kufuata maadili ya utumishi wa umma, hatua kali stahiki zitachukuliwa juu yake na hakutakuwa na muda wa kuvumilia au kufumbia macho vitendo vya ukosefu wa uadilifu.

Akifunga semina hiyo, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa ,  Tumsifu Zakayo ametumia nafasi hiyo kuwataka watumishi  kufanyia kazi yote yaliyosemwa na wawezeshaji wa semina hiyo na kurekebisha makosa ili kulinda taswira ya Chuo na utumishi wa umma  kwa ujumla.

Semina hii imefanyika kwa watumishi katika Ndaki, Shule Kuu, Taasisi na Idara mbalimbali za UDOM kuanzia tarehe 13 - 19 Novemba, 2023.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com