WENYE MAHITAJI MAALUM WAKUMBUKWA UDOM



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM)kimezindua Harambee ya kuwachangia wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma chuoni hapo ili kuchochea ari ya mafanikio yao ikiwa ni pamoja na kuongeza ushawishi kwa wanafunzi wengine wa kundi hilo kutokata tamaa ya kusoma. 

Hayo yamejiri November 29,2023 Jijini hapa kwenye Mkutano wa 14 wa Baraza la wahitimu wa Chuo hicho (UDOM) ambapo fedha zitazopatikana kupitia Harambee hiyo zitasaidia kukidhi mahitaji ya ada, magongo,vifaa wezeshi na mengineyo. 

Akizungumza kwenye Baraza hilo, Waziri wa Madini nchini Peter Mavunde ameipongeza hatua hiyo huku akitoa maelekezo kwa Uongozi wa UDOM kuandaa orodha ya wadau wa Chuo hicho na kuwaomba kuchangia ili kufikia malengo kwa kuwa kila mwenye ulemavu ana haki ya kuishi maisha mazuri.

Kwa kutambua umuhimu wa wenye mahitaji maalum Mavunde kwa upande wake amechangia shilingi milioni tano za kitanzania ambazo zitasaidia kuboresha baadhi ya mahitaji kwa wanafunzi hao.

"Mnatambua hapa nimemwakilisha Naibu Waziri Mkuu ambaye hajaweza kufika hapa kutokana na kuwa na majukumu mengine, yeye kwa upande wake ameahidi kutoa shilingi milioni kumi,na mimi binafsi natoa milioni tano naamini kabisa hii itaweza kusaidia kwa kiasi fulani," amesema

Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa UDOM anayeshughulikia Mipango,Fedha na Utawala Prof.Winesta Anderson ameeleza kuwa Chuo hicho kina jumla ya wanafunzi 160 wenye mahitaji maalumu . 

Amefafanua kuwa kati yao wenye uoni hafifu ni 12,walemavu wa ngozi 28,wenye ulemavu wa kutosikia ni 70 na wengine 46 waliosalia wapo kwenye kundi la ulemavu mwingine. 

"Amesema msingi wa jumuiya ya Tanzania unamtaka kila mwananchi kupata elimu bila kujali hali yake na kwamba kwa kulitambua hilo wao kama wadau wana mpango mkakati wake ambao utakamilika 2026 ukiwa umezingatia kwa undani mahitaji ya wanafunzi hao" amesema na kuongeza;

"UDOM kupitia convocation hii tumesema tulilete hili kama kampeni ya kuwasaidia wenye uhitaji kusoma na kufika chuo Kikuu,Wizara yetu mama ya elimu imeendelea kitusapoti kwa kutupatia bajaji nane,laptop 26, mafuta na bado tunaendelea kunapambana kuhakikisha kila sehemu inapitika ili wanafunzi wetu wawe salama,"amesema

Naye Mlezi wa wanafunzi wenye mahitaji maalum chuoni hapo kupitia Kurugenzi ya huduma za wanafunzi    Florida  Chambi ameeleza kuwa ili kufanikiwa katika kampeni hiyo,kiasi cha shilingi milioni 300 kinahitajika ambacho kitakusanywa kwa kipindi cha miezi 12 kuanzia sasa. 

Amesema fedha hizo zitasaidia pia kuboresha hali ya miundombinu ya wanafunzi hao ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya vyumba wanavyolala kuendana na hali yao. 

"Tunaishukuru Serikaki na Chuo hiki kwa jitihada zake mfano, Chuo kimeendelea kuwajali wanafunzi hawa kwa kuajiri madereva maalum wanaweza kuendesha bajaji na kuwarahisishia usafiri, Chuo pia kimetoa motisha kwa wanafunzi wanaowasaidia wenye mahitaji maalum kama Shukrani kwa kuwawekea mazingir wezeshi, "amesema

Chambi amesema Chuo hicho kinajali kuwatengea wanafunzi wenye mahitaji maalumu chumba cha mtihani na kueleza kuwa kupitia kurugenzi hiyo wanaendelea kuboresha zaidi kila eneo ili kuwawezesha wanafunzi hao kusoma kwa bidii kufikia malengo yao. 

Pamoja na hayo baadhi  ya wadau wa UDOM wameweza kuchangia harambee hiyo akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ambaye ameahidi milioni mbili,Ridhiwan Kikwete milioni mbili,Kituo cha uwekezaji million mbili huku Makamu mkuu wa Chuo hicho Prof.Lughano Kusiluka akiahidi kuchangia shilingi milioni mbili. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post