Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Serikali kupitia wizara ya Fedha imekusudia kutekeleza kwa nguvu mpango mkuu wa maendeleo ya sekta ya Fedha wa mwaka 2020/2021/2029/2030 ambapo ifikapo mwaka 2025 takribani Asilimia 80 ya wananchi watakuwa wamepata uelewa wa Masuala ya fedha.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Katibu Mkuu wizara ya Fedha, kamishna Mwamwaja wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuhusu Madhimisho ya wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa ambayo yanatarajiwa kufanyika Jijini Arusha Tarehe 20 na 26 Novemba 2023 katika viwanja vya Shekhe Amri Abeid.
Kamishna Mwamwaja amesema lengo la wiki ya huduma za Fedha ni kujenga uelewa na weledi kwa Umma katika matumizi ya sahihi ya huduma za Fedha zinazotolewa ili kujenga Uchumi na kuondoa umaskini na kutarajiwa kuwa na matokeo chanya Kwa mtu binafsi,kaya, jamii na Taifa kwa ujumla ili kuongezeka Kwa idadi ya watu wenye kiwango cha ufahamu wa Elimu ya Fedha na maarifa Juu ya upatikanaji na utumiaji wa bidhaa na huduma Rasmi za kifedha.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa wiki ya huduma za fedha unatarajiwa kuwa na matokeo chanya kwa mtu binafsi,kaya,jamii na taifa kwa ujumla kwa kuongezeka kwa idadi ya watu wenye kiwango cha ufahamu wa elimu ya fedha na maarifa juu ya upatikanaji na utumiaji wa bidhaa na huduma rasmi za kifedha,kuimarika kwa uelewa na matumizi ya masoko ya fedha.
"Kupitia wiki ya huduma tutaweza kusogeza huduma za fedha karibu zaidi na wananchi,kuimarisha matumizi ya huduma hizo pamoja na kupata maoni na ushauri wa kuboresha huduma hizo,kuwawezesha watumiaji wa huduma za fedha kuelewa haki na wajibu wao,kuwawezesha wananchi kupata maarifa kuhusu namna bora ya kusimamia vizuri rasiliamali fedha pamoja na kuwaunganisha wajasiriamali,"ameeleza
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi idara ya Uendelezaji wa Sekta ya fedha Dionisia Mjema ameeleza kuwa fursa mbalimbali zinazotolewa na sekta hiyo ni pamoja na kukuza na kuimarisha biashara kwa wananchi na kupata maarifa na uelewa wa masuala ya fedha na hivyo kuwezesha kujenga utamaduni wa kutumia huduma rasmi za kifedha na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi.
"Kutokana na utafiti wa Finscope wa mwaka 2023 inaonesha nchini Tanzania ni asilimia 53.8 tu ya nguvu kazi wanatumia huduma rasmi za fedha na hivyo kubaki na kundi kubwa la watanzania ambao hawafaidiki na huduma hizo na kukosa fursa za kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za uchumi ambazo zingewezesha kuchangia katika kukuza pato la taifa, "amesema
Madhimisho ya wiki ya huduma za Fedha Kitaifa yamepangwa kufanyika katika viwanja vya sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuanzia tarehe 20 mpaka 26 Novemba 2023 yakiongozwa na kauli mbiu isemayo "ELIMU YA FEDHA, MSINGI WA MAENDELEO YA KIUCHUMI"
Social Plugin