Mazishi ya mwili wa mwendeshaji na Mmiliki wa Mtandao wa MASWA YETU BLOG, Innocent Lugano Mbwaga (30) maarufu Blogger Boy yamefanyika leo Jumatatu Desemba 11,2023 katika makaburi ya Roma Mjini Maswa Mkoani Simiyu.
Mazishi ya Innocent yamehudhuriwa na waombolezaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Simiyu wakiongozwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba Bi. Mariam Mwanzalima.
Innocent Mkazi wa Maswa Mkoani Simiyu ambaye alikuwa Afisa Lishe Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara alifariki dunia Desemba 8,2023 wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Kanda ya Kusini - Mtwara baada ya kupata ajali ya pikipiki aliyokuwa anaendesha Tandahimba Desemba 5,2023.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba Bi. Mariam Mwanzalima amesema Innocent Mbwaga aliajiriwa na Halmashauri ya Wilaya Tandahimba tarehe 14/06/2023 kwa Cheo Afisa Lishe II, alikuwa kijana mchapakazi, hodari mwenye nidhamu ya kiutumishi na alikuwa na ushirikiano na watumishi wenzake na jamii kwa ujumla.
"Ninatoa pole kwa Familia ya marehemu, watumishi wa Halmashauri ya Tandahimba, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu",amesema Mwanzalima.
"Huu ni msiba ni mzito sana kwa wamiliki na waendeshaji wa mitandao ya kijamii, tumepoteza kijana shupavu sana, mtu bingwa sana aliyetumia muda mwingi kusaidia vijana mtandaoni..Tumepoteza Blogger mkubwa Kanda ya Ziwa, tumepoteza Blogger mkubwa Tanzania.
Tumepoteza gwiji wa masuala Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, tumepoteza mwalimu wa Bloggers Tanzania, mwalimu wa Digitali, tumepoteza Bingwa wa TEHAMA, tumepoteza rafiki, tumepoteza ndugu, tumepoteza mtu muhimu sana... alitumika kama daraja la vijana wengi kwa kuwapa msaada namna ya kuomba kujiunga na vyuo mbalimbali hapa nchini. Pumzika kwa amani kaka Innocent Lugano Mbwaga.. ulipenda kuitwa Blogger Boy au Adsence Officer Tanzania", amesema Kadama Malunde, mmiliki na Mkurugenzi wa Mtandao wa Malunde 1 blog.
Innocent Mbwaga alizaliwa tarehe 29/12/1993 katika Wilaya ya Maswa Mkoa wa Simiyu na kufariki dunia Desemba 08,2023.
Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Shanwa na kujiunga na kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Binza na kuhitimu kidato cha nne mwaka 2010. Mwaka 2011 alijiunga kidato cha tano shule ya Sekondari Ngudu na kuhitimu kidato cha sita 2013.
Baada ya kuhitimu shahada ya Sayansi ya chakula na Teknolojia (Bsc. Food Science and Technology) katika chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine Morogoro kuanzia 2013 na kuhitimu 2016, alijikita katika shughuli mbalimbli ili aweze kujipatia kipato ikiwemo kufundisha shule za Sekondari huku akijihusisha na masuala Teknolojia ya Habari na Mawasiliano akiendesha mitandao ya kijamii ukiwemo mtandao wake wa Maswa Yetu Blog.
Baadaye alihamia Mkoa wa Kilimanjaro ambapo alijishughulisha na ufundishaji katika shule ya sekondari ya wasichana Machame na kuendesha pikipiki (bodaboda) hadi mwaka 2023.
Innocent Mbwaga aliajiriwa na Halmashauri ya Wilaya Tandahimba Tarehe 14/06/2023 kwa Cheo Afisa Lishe II.
Mpaka umauti unamfika marehemu alikuwa anafanya kazi kama Afisa Lishe II Katika Idara ya Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara.
"Raha ya Milele Umpe ee Bwana Na Mwanga wa Milele Umuangazie Marehemu Apumzike kwa Amani" ,Amina.
Mmiliki na Mkurugenzi wa Mtandao wa Malunde 1 blog, Kadama Malunde akiwa ameshikilia picha ya marehemu Innocent Mbwaga ' Blogger Boy'
Social Plugin