Mshindi wa Kwanza wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi / Jua Kali, Dkt. Herieth Mkanga (katikati) anayejishughulisha na utengenezaji wa Batiki aliyejipatia umaarufu kwa kutengeneza vazi maarufu linalojulikana kama Suti ya Samia akiwa kwenye picha ya pamoja na washindi wenzake kutoka Tanzania Bi. Asha Rutta (kulia) ambaye alikuwa mshindi wa pili na Bi. Mwanahamisi Rashidi mshindi wa tatu (3) kwa mabanda ya wajasiriamali kutoka Tanzania.
Na; Mwandishi Wetu - Bujumbura BURUNDI
Mjasiriamali kutoka Tanzania ameibuka mshindi wa kwanza wa jumla kwenye Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Nguvu Kazi/Juakali yaliyomalizika jijini Bujumbura, Burundi leo tarehe 15 Desemba 2023.
Mshindi wa pili ametokea Kenya huku mshindi wa tatu akitokea Uganda.
Mjasiriamali huyo, Dkt. Herieth Mkanga anayejishughulisha na utengenezaji wa Batiki ameibuka mshindi kwa kutengeneza vazi maarufu la “Suti ya Samia” ikiashiria mtindo wa nguo unaopendelewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Dkt. Mkanga amesema kuwa amefurahia ushindi huo ambao ni mkubwa kwake na kwa Tanzania na kwamba tuzo hiyo ni chachu kwake ya kuendelea kujituma zaidi na kutengeneza bidhaa nyingi na zenye ubora ili kulikamata soko la Afrika Mashariki, Afrika na Duniani kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Ajira, Bi. Kissa Kilindu amewahamasisha wajasiriamali kote nchini kujiamini na kuchangamkia fursa mbalimbali za biashara, masoko na uwekezaji zinazotangazwa na Serikali ndani na nje ya nchi.
Wakati huohuo, Wajasiriamali wawili wenye ulemavu wa macho kutoka Zanzibar, Bw. Abdul Kadir Amini Ahmed na Bw. Khamis Khamis Haji wanaojishughulisha na utenegenezaji wa mikeka wamepongezwa na waandaji wa maonesho hayo kwa kufanikiwa kushiriki maonesho hayo kikamilifu licha ya hali ya ulemavu waliyo nayo huku jamii ikitakiwa kuiga mfano wao wa kujituma katika kazi badala ya kutegemea kuomba kusaidiwa.
Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo yamebeba Kaulimbiu isemayo “Kuunganisha Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki kufanya biashara katika Eneo la Afrika Mashariki” hufanyika kila mwaka kwa utaratibu wa mzunguko kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine ambapo maonesho ya 24 yanatarajiwa kufanyika nchini Sudan Kusini mwaka 2024.
Mshindi wa Kwanza wa Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi / Jua Kali, Dkt. Herieth Mkanga (katikati) anayejishughulisha na utengenezaji wa Batiki aliyejipatia umaarufu kwa kutengeneza vazi maarufu linalojulikana kama Suti ya Samia akiwa kwenye picha ya pamoja na washindi wenzake kutoka Tanzania Bi. Asha Rutta (kulia) ambaye alikuwa mshindi wa pili na Bi. Mwanahamisi Rashidi mshindi wa tatu (3) kwa mabanda ya wajasiriamali kutoka Tanzania.
Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Ajira, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Kissa Kilindu akizungumza wakati wa hafla ya kufunga Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi / Jua Kali yanayofanyika jijini Bujumbura leo tarehe 10 Desemba, 2023.
Shamrashamra za baadhi ya Wajasiriamali baada ya Tanzania kutoa Mjasiriamali ambaye amekuwa mshindi katika Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi / Jua Kali yaliyofanyika jijini Bujumbura leo tarehe 15 Desemba, 2023.
Waziri wa Viwanda, Biashara, Uchukuzi na Utalii Burundi, Mhe. Nijimbere Marie Chantal (kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajasiriamali wasiiona Bw. Abdul Kadir Ahmed (kulia) na Bw. Khamis Haji (katikati) wakati wa hafla ya kufunga maonesho ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika maarufu Nguvu Kazi / Jua Kali yanayofanyika katika viwanja vya Cercle Hyppique, jiji la Bujumbura nchini Burundi.
Social Plugin