MBUNGE CONCHESTA LEONCE RWAMLAZA AGAWA MITUNGI YA GESI KAGERA





Na Mariam Kagenda _ Kagera

Mbunge wa viti maalum Mkoani Kagera  Mhe, Conchesta Leonce Rwamlaza ametimiza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan la ugawaji wa mitungi ya gesi kwa Wanawake wa kata za Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba wanaokwenda kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
 

Akizungumza kabla ya zoezi la ugawaji wa mitungi  75 kwa akina Mama waliofika na kuwakilisha wenzao kutoka baadhi ya kata hizo ikiwemo kata ya Kyaitoke, Kyamulaile Katoma Nyakato na nyinginezo Mbunge Rwamlaza amempongeza Rais Samia kwa namna alivyowaunga mkono wabunge wa Tanzania  kuhusu matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia na kuwafanya wabunge hao kuwa waratibu wa ugawaji wa mitungi hiyo jambo litakalosaidia akina Mama hao kuondokana na madhara yanayoweza kutokana na kupika kwa kutumia kuni na mkaa.

Rwamlaza amesema yeye kama mbunge wa viti maalum kutoka mkoa wa Kagera kupitia CHADEMA anamuunga mkono Rais Samia kupitia mabadiliko ya Nchi kuongozwa na Mwanamke na kuwa ukiachana na itikadi za vyama Rais Samia amefanya jambo kubwa na la kihistoria.

"Rais Samia ni Mama mpambanaji nani asiyejua kuwa kawezesha miradi mingi na mikubwa hapa nchini tumeona katika sekta ya Elimu Barabara, afya na nyinginezo hivyo mimi  siangalii mambo ya vyama ninachoangalia ni namna anavyowapigania wanyonge kama ambavyo amewainua Wanawake hawa", alisema Mbunge huyo.

Ameongeza kuwa huu ni muda wa akina Mama hao kupika kwa urahisi bila vikwazo kwani awali waliotumia kuni walihusishwa katika imani za kishirikina baada ya macho yao kuonekana mekundu huku akiwahimiza kuitumia mitungi hiyo kwa lengo lililokusudiwa   kwani nia ya Rais Samia ni njema kwao.

Mitungi hiyo imegawiwa kidogo kwa  watu wawili wawili kila kata ili wawe mabalozi kwa wengine kutumia na kuchochea matumizi sahihi ya nishati safi na salama ya kupikia.

Naye Mgeni rasmi katika zoezi hilo ambaye ni mratibu wa miradi ya REA Wilaya ya Bukoba Bi Jamila Haroub Juma akitoa darasa na namna ya matumizi sahihi ya mitungi hiyo amesema mitungi hiyo imetolewa mahususi kuhamasisha kutumia nishati safi na salama ya kupikia na imetolewa na Wakala wa nishati Vijijini (REA) kwa kupata ruzuku kutoka Serikali kuu ambapo Rais Samia amewaondolea changamoto za kiafya zitokanazo na moshi kwani wengine ujikuta wanapata madhara kwenye mapafu, kifua kutokana na kuvuta hewa chafu.

Aidha Jamila amewahimiza akina mama hao kutunza, kutumia na kuendeleza mitungi hiyo wala si kwa matumizi mengine kwani watakuwa wamekwenda tofauti na dhamira ya Serikali.

"Mnatakiwa kurudisha shukrani kwa kutumia  nishati hii ili kuepukana na madhara yatokanayo na moshi utokanao na mkaa na kuni tumeona watu wakipata shida kwenye  mapafu kutokana na kuvuta hewa chafu hivyo nimpongeze Rais Samia kuwezesha zoezi hilo ambalo litakuwa endelevu kwa nchi nzima",amesema.

Hata hivyo akina Mama hao akiwemo Bi Winifrida Maxmilian  wa kata Katoma, Hildagarda Ponsian wa kata Nyakato na Bi Ashura Jafari kutoka Kyaitoke Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba wamemshukuru Rais Samia kupitia mbunge huyo viti maalum Bi Rwamlaza na kuwa mradi huo utawasaidia kutunza Mazingira kwa kutokata miti ovyo kwa ajili ya kupata kuni na mkaa ambapo pia Rais Samia amewaweka katika maisha ya kati huku wakiahidi kutumia vyema mitungi hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post