Na Vera Assenga - Dar es salaam
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeshiriki katika uzinduzi wa sera ya kijinsia ya Chama Cha Kijamii (CCK) yenye lengo la kuleta usawa kwa taifa katika kuwapata viongozi wenye kuleta tija kwa Taifa kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.
Uzinduzi huo uliofanyika leo Desemba 15,2023 Jijini Dar es salaam umekuja baada ya Chama hicho cha siasa cha CCK kupokea mafunzo kutoka TGNP na WiLDAF Novemba 2021 - Septemba 2022 ya jinsi gani wanaweza kuingiza masuala ya jinsia katika sera, mipango na miongozo yao ambapo CCK ni miongoni mwa vyama nane vya siasa vilivyowezeshwa kutengeneza sera ya kijinsia ya vyama vya siasa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mama Gemma Akilimali amesema, “Kwetu sisi hatua waliyofikia CCK ni ya kupongezwa sana kwa kuwa wameonyesha dhamira ya dhati katika kuweka mazingira ya kuhakikisha ongezeko la wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi na maamuzi”.
Naye Mwenyekiti wa CCK, David Daudi ameishukuru TGNP kwa kuwapa elimu na kuwawezesha mpaka leo wameweza kuzindua sera yao ya kijinsia.
Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP Mama Gemma Akilimali akizungumza wakati wa uzinduzi huo