NA MWANDISHI WETU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) pamoja na wadau wengine kwa kuiunga mkono Serikali kwa mchango wa namna mbalimbali ili kuendeleza mapambano ya kutokomeza Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI.
Pia amewahakikisha wadau hao kwamba serikali itaendelea kuunga mono jitihada zinazooneshwa na GGML na wadau wengine katika kukabiliana na janga hilo la UKIMWI nchini.
Majaliwa ametoa kauli hiyo jana tarehe 1 Disemba wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya UKIMWI duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya sekondari ya Morogoro, mjini Morogoro.
“Nitambue mchango wa sekta binafsi na taasisi mbalimbali na wadau wa maendeleo ndani na nje ya nchi katika mapambano dhidi ya UKIMWI na hakika mafanikio haya tuliyoyatamka hapa yanatokana na ushiriki wenu ninyi wadau.
“Hivyo natoa shukrani nyingi za dhati sana kwenu kwani nyie wadau muhimu kwa maendeleo ya vita hii naamini tukiendelea kuungana pamoja na serikali yetu tutafikia malengo yetu, vilevile niwahakikishie kwamba serikali yenu itaendelea kuunga mkono jitihada hizi za kutokomeza VVU/ UKIMWI hapa nchini,” alisema Majaliwa
Aidha, alisema anatambua mafanikio ya kutokomeza janga hilo yametokana na jitihada za wadau hao ikiwamo GGML.
“Niupongeze na kuushukuru Mgodi wa Geita Gold Mining Limite (GGML) kwa jitihada zake, tunashukuru sana kwa kuunga mkono kwenye ufadhili wa afua za VVU/ UKIMWI hapa Tanzania,” alisema Majaliwa.
Kutokana na jitihada hizo katika maadhimisho hayo, Majaliwa alitunuku cheti GGML kutokana ufadhili wake kwenye Mfuko wa Udhamini wa Ukimwi (ATF) ambacho kilipokelewa na Meneja Mwandamizi wa Afya, Usalama na Mazingira wa GGML, Dk. Kiva Mvungi.
Dk. Kiva mbali na kuishukuru Serikali kwa kutambua jitihada za kampuni hiyo, alisema dhamira ya GGML ni kuendeleza jitihada za mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ambazo kampuni hiyo kila mwaka hufanya kupitia kampeni ya GGM Kili Challenge na mwaka huu imechangia Sh milioni 100.
Kampeni hiyo ambayo iliasisiwa mwaka 2002, hushirikisha wapanda mlima Kilimanjaro kwa njia ya miguu na baiskeli kwa lengo la kuchangisha fedha za kutunisha mfuko wa mapambano ya Ukimwi (ATF), kuwezesha upatikanaji wa afua mbalimbali pamoja na kuwezesha taasisi binafsi zinazojihusisha na vita dhidi ya janga hilo.
Hadi sasa kampeni hii imesaidia miradi zaidi ya 100 nchini kote tangu kuanzishwa kwake mwaka 2002.
Awali Majaliwa alizindua ripoti ya utafiti wa viashiria vya Ukimwi ambayo inaonesha maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua.
“Maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua kutoka watu 72,000 waliokuwepo mwaka 2016/2017 hadi watu 60,000 kwa mwaka 2022/2023. Hii ni sawa upungufu wa asilimia 0.18 ambapo asilimia 0.24 ni wanawake na asilimia 0.11 ni wanaume,” alisema.
Amesema Serikali iliamua kufanya utafiti kwa lengo la kujua hali ya sasa ya VVU na Ukimwi ilivyo hapa nchini na matokeo yameonesha kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Social Plugin