ASKOFU SANGU : KANISA KATOLIKI HALIJAWAHI KUHALALISHA NDOA ZA JINSI MOJA... MSIMAMO WA KANISA NDOA NI KATI YA MKE NA MME TU SI VINGINEVYO


Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amesema Kanisa halijawahi kufundisha au kuhalalisha muungano wa kindoa kati ya watu wa Jinsi moja.

Kupitia salamu zake za Krismasi na mwaka mpya wa 2024 alizozitoa kwa Wakristo na watu wote amebainisha kuwa, madai hayo yanatokana na upotoshwaji mkubwa wa makusudi kuhusu mafundisho ya Kanisa Katoliki, ambapo baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa na kasi kubwa ya kuandaa akaunti za uongo na kuweka taarifa zinazopotosha msimamo wa Kanisa, juu ya muungano hasi wa ndoa za jinsi moja.

Askofu Sangu amefafanua kuwa, msimamo na mafundisho ya Kanisa Katoliki mpaka sasa unabaki kuwa ndoa ni kati ya Mke na Mme na wala si vinginevyo, na linasisitiza kuwa hakuna ndoa inayohusisha watu wa jinsia moja kwa kuwa jambo hilo ni kinyume na mafundisho ya neno la Mungu, mila na desturi za Kiafrika, kinyume cha sheria za Tanzania na ni kinyume cha sheria ya asili ya maumbile (Natural law)

“Nyakati zetu hizi tunashuhudia upotoshwaji mkubwa na wa maksudi kuhusu mafundisho ya Kanisa Takatifu la Mungu. Tumeshuhudia baadhi ya vyombo vya Habari vimekuwa na kasi kubwa ya kuandaliwa kwa akaunti za uongo na kuweka taarifa potoshi, mintarafu msimamo wa Kanisa Katoliki juu ya muungano hasi wa jinsi moja.

Ukweli ni kwamba Kanisa Katoliki halijawahi, kamwe kufundisha au kuhalalisha muungano wa kindoa kati ya watu wa jinsi moja. Huu ni upotoshaji ulioghubikwa na hila za Ibilisi aliye mwovu.

Kanisa linasisitiza kwenye mafundisho yake kuwa ndoa ni kati ya Mke na Mme na si vinginevyo, na linasisitiza hakuna ndoa inayohusisha watu wa jinsi moja na kwamba ndoa za jinsia moja ni kinyume na mafundisho ya neno la Mungu, mila na desturi zetu za Kiafrika, kinyume cha sheria zetu za Tanzania na ni kinyume cha sheria ya maumbile (Natural law)

Askofu Sangu amesisitiza kwamba, Kanisa Katoliki linaamini kuwa ni dhambi kubwa kwa wanaoishi maisha ya jinsi hiyo, kwa wanaoshabikia na kwa wale wanaohamasisha kwa namna yoyote ile.

Askofu Sangu amewatahadharisha wakristo pamoja na jamii nzima kuwa makini na vyombo mbalimbali vya habari ambavyo vinajaribu kupotosha kwa lengo la kuwafanya Wakristo wayaache mafundisho sahihi ya Kimungu.

Wakati huohuo, Askofu Sangu amezishauri mamlaka za Serikali hapa nchini kutilia mkazo suala la uwepo wa vipindi vya dini kwa wanafunzi wawapo shuleni, ili wapate mafundisho sahihi juu ya Imani na kulifanya taifa kuwa na watu wenye hofu ya Mungu, hatua ambayo itasaidia kuwa na viongozi waadilifu, wazalendo na ambao hawatakuwa tayari kuuza utu na heshima ya wanaowaongoza kwa lengo la kujitafutia umahiri bandia na kujinufaisha binafsi kwa gharama za wengine.

Aidha amewaomba Watanzania wote kuendelea kuliombea taifa na hasa viongozi waendelee kuwa na hofu ya Mungu, ili Taifa lidumu na kustawi katika Haki, Amani, Upendo na Mshikamano wa kweli .

Leo, Wakristo kote duniani waadhimisha sikukuu ya Krismasi, ambayo ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mkombozi wao Yesu Kristo.

Chanzo - Radio Faraja Fm website

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post