Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHUWASA YAFANYA UKARABATI WA MADARASA SHULE YA MSINGI JOMU



Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga SHUWASA imefanya ukarabati wa madarasa matatu katika shule ya msingi Jomu iliyopo kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga kwa lengo la kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi wa walimu wakati wawapo shuleni.

Makabidhiano ya madarasa hayo yaliyokarabatiwa yamefanyika leo Desemba 7, 2024 katika shule ya msingi Jomu.

Akizungumza wakati wa hafla fupi makabidhiano ya madarasa hayo Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Jomu Pendo Peter amesema kufuatia ukarabati wa madarasa matatu kwenye shule hiyo imeweza kuchangia ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi ukilinganisha na hapo awali.

"Kukamilika kwa ukarabati wa madarasa haya imechangia ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi na kuleta motisha kwa walimu katika ufundishaji, hapo awali hali ya miundombinu ilikua si rafiki lakini kwa sasa tunawashukuru wadau wa elimu ikiwemo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga SHUWASA kwa kufanya ukarabati huu mkubwa", amesema Mwalimu Pendo Peter.

Kwa upande wake afisa elimu wilaya ya Shinyanga Marry Maka amewapongeza SHUWASA kwa hatua waliochukua na kuwaomba wadau wengine kuiga mfano kwa kuendelea kujitokeza kuchangia sekta ya elimu  katika shule mbalimbali ndani ya wilaya ya Shinyanga.


"Niwapongeze sana Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga SHUWASA kwa mchango mkubwa walioutoa kwe nye sekta ya elimu katika shule hii ya Jomu, kwa kufanya hivi tunawatia moyo  wanafunzi kuendelea kufanya vizuri kwenye masomo kwa kuwawekea mazingira mazuri pindi wawapo shuleni, niwaombe na wadau wengine waige mfano kama huu", amesema Marry Maka.

Diwani wa kata ya Kambarage Hassani Mwendapole wamewapongeza waalimu na wanafunzi kwa kuongeza kiwango cha ufaulu shuleni hapo na kutoa wito kwa wazazi na walezi kusimamia malezi kwa watoto wao katika kipindi hiki cha likizo kwa wanafunzi

"Tumeshuhudia ni namna mara baada ya ukarabati huu watoto wetu wamekuwa wakifanya vizuri kwenye masomo yao hii ni juhudi kubwa iliyofanywa na waalimu wetu katika ufundishaji darasani na wadau wetu wanaoendelea kuishika mkono serikali yetu, lakini pia serikali ya awamu ya sita kupitia Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hasan ilitupatia shilingi milioni 100 kwaajili ya ujenzi wa madarasa ya uviko 19 katika shule hii",

"Niwasihi wazazi na walezi waangalieni watoto katika kipindi hiki cha likizo ili watakaporudi shuleni waendelee kufanya vizuri, Kama alivyosema afisa elimu wilaya na mimi nitoe wito kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia taasisi zetu ikiwemo shule ya msingi Kambarage", amesema Diwani Mwendapole.


Akieleza gharama za ukarabati wa madarasa hayo Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola amesema kuwa ukarabati huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 3.35 uliohusisha ukarabati wa madarasa matatu ya shule hiyo.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya madarasa hayo.


Madarasa yaliyofanyiwa ukarabati









Mwenyekiti wa Kamati ya Shule Sose Malongo akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano.

Afisa Elimu kata ya Mjini Elizabeth Mboje akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano.

Mwalimu wa shule ya msingi Jomu Masanja Ezekiel akitoa shukrani kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira SHUWASA kwa kufanya ukarabati wa madarasa hayo.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Jomu Pendo Peter akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano.
Mmoja wa wazazi akizungumza wakati wa hafla hiyo ya makabidhiano.
Picha ya makabidhiano ya madarasa hayo.
Picha ya pamoja.

Picha ya pamoja na walimu wa Shule ya Msingi Jomu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com