Na Elizabeth John, LUDEWA.
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa Mkoa wa Njombe, Victoria Mwanziva amefanya ziara ya kimkakati ya ukaguzi wa miradi ya maji Wilayani Ludewa inayotekelezwa kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 13 na kutoa onyo kwa wananchi wanaoshindwa kutii sheria zinazokataza kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo vya maji.
Mwanziva amesema kuwa lengo la ziara yake katika miradi ya maji ni kuhakikisha kuwa wakazi wa Ludewa wanapata huduma ya maji bora, safi, salama na yenye kutosheleza,sambamba na kuonesha kazi kubwa inayofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya maji wilayani humo.
“Adhma ya Mh. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan juu ya kumtua mama ndoo kichwani ipo palepale, hivyo basi naomba nitoe wito kwa wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji, uelimishwaji wa jamii juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji uwepo ili vinufaishe vizazi vijavyo sambamba na kutunza miundombinu yote ya maji,” amesema Mwanziva.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Sunday Deogratius amezungumzia suala la usimamizi wa utunzaji wa mazingira kwenye vyanzo vya maji, amesema tayari halmashauri imetunga sheria ndogo.
“Mkuu wa wilaya sisi tayari tumeshatunga sheria ndogo za usimamizi wa vyanzo vya maji, hatutasita na kuchukua hatua kwa wale ambao watakaidi kwa sababu tuna amini maji ni uhai, maji ni maisha,” amesema Deogratius.
Mwenyekiti wa kijiji cha Ludewa, Wilfred Mwalongo ameishukuru serikali kwa hatua kubwa ya kupeleka maji kwenye eneo lao kwa sababu kumepunguza pia changamoto ya ndoa nyingi kuvunjika.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Ludewa mjini, Mhandisi Enock Ngoyinde akitoa taarifa, alisema kuwa katika mradi wa maji wa kitongoji cha Kilimahewa kata ya Ludewa tayari kuna mradi wa maji wa matenki mawili unaosaidia kupatikana kwa maji safi na salama kwa gharama ya shilingi bilioni saba.