Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeshika nafasi ya Pili na kunyakua tuzo ya umahiri katika utayarishaji bora wa taarifa za hesabu kwa mwaka 2022/2023 kwa kufuata viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu International Public Sectors Accounting Standards (IPSAS) katika kundi la Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.
Tuzo hiyo imetolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) katika hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha NBAA APC hotel Bunju jijini Dar es Salaam.
Kutokana na mafanikio ya tuzo hiyo, Kamishna wa Mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya Tanzania Areta Lyimo amekipongeza Kitengo cha fedha na uhasibu na idara nyingine ndani ya mamlaka kwa kufanikisha uandaaji bora wa hesabu uliopelekea kuwa washindi wa tuzo hiyo.
“Uandaaji bora wa taarifa za hesabu ni moja ya ufanisi wa ofisi yoyote hivyo nawapongeza sana Kitengo cha fedha na Uhasibu pamoja na idara nyingine kwa kutoa mchango mkubwa kuhakikisha Kitengo cha fedha na uhasibu kinafanya vizuri” amesema kamishna Lyimo
Kamishna Lyimo amesema ushindi huo umetokana na ushirikiano wa divisheni, vitengo, na sehemu zote za Mamlaka. Hivyo amewaomba watumishi kuendelea kuchapa kazi ili Mamlaka iendelee kung’ara.
Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA)) hutoa tuzo hizi kila mwaka kwa kushindanisha wizara, taasisi, mashirika, na kampuni mbalimbali nchi nzima.
Social Plugin