Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao(e-GA)Mhandisi Benedict Ndomba amesema Mamlaka hiyo inaendelea kutekekeza agizo la Serikali la kuhakikisha mifumo ya TEHAMA katika Taasisi za umma zinasomana kwa kuuganishwa na kubadilishana taarifa kidijitali.
Katika kutekeleza hilo amesema,Mamlaka imefanikiwa kujenga mifumo mitatu ambayo ni mfumo Mkuu wa ubadilishaji taarifa Serikalini(GovESB), Mfumo wa pamoja wa kielekroniki wa uondoshaji wa shehena maeneo ya forodha(TeSWS)pamoja na Mfumo wa ubadilishanaji taarifa kati ya TEHAMA ya Serikali na ya Sekta binafsi.
Mkurugenzi huyo ameeleza hayo leo Desemba 22,2023 Jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa jitihada za mifumo ya TEHAMA ya taasisi za umma katika kubadilishana taarifa kidijitali ili kuzungumza lugha moja ya kimtandao.
Akizungumzia kuhusu mfumo wa GovESB amesema hadi sasa jumla ya taasisi za umma 109 zimeunganishwa katika mfumo huo huku mifumo 117 imesajiliwa na miongoni mwa taasisi hizo ni mamlaka ya vitambulisho vya Taifa(NIDA),wakala wa leseni za biashara (BRELLA),Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) na zinginezo.
"Pamoja na kutekeleza agizo la Rais Samia,mfumo huu umetengenezwa kwa kuzingatia kifungu cha 48(2)cha sheria ya serikali mtandao Na.10 ya mwaka 2019 kinachoitaka mamlaka hiyo kuanzisha na kuendesha mfumo unaowezesha mifumo ya TEHAMA Serikalini kuwasiliana na kubadilishana taarifa,"amesema na kuongeza;
Lengo la Mfumo huo ni kuziwezesha taasisi za umma kubadilishana taarifa kidijitali kwa usalama,kupunguza urudufu wa mifumo,kuongeza ufanisi wa utendaji kazi,kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuokoa muda kwakuwa taarifa hupatikana kwa wakati, "amesema
Amesema kabla ya kuanza kwa mfumo wa GoVESB kulikuwa na changamoto mbalimbali za ubadilishaji wa taarifa katika taasisi za umma,zikiwemo kutumia muda mrefu kupata taarifa kwani taasisi zililazimika kuwasilisha maombi ya kupata taarifa inazohitaji kwa njia ya barua katika taasisi husika na kwamba uaratibu huo ulichukua muda mrefu jambo lilichangia kupunguza ufanisi katika utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
"Awali ili mifumo ya TEHAMA iweze kusomana ililazimika kuinganisha mfumo mmoja kuzungumza na mifumo mingine kila inapohitajika ambapo amesema uunganishwaji huo ulisababisha urudufu wa mifumo,kupungua kwa usalama,kupunguza ufanisi wa mifumo na kuongeza gharama za usimamizi na uendeshaji wa mifumo ya TEHAMA,
"Kupitia GoVESB changamoto hizo zimetatuliwa na sasa taasisi zote zinabadilishana taarifa kupitia mfumo huu hupata taarifa zinazohitajika kwa wakati na kwa usalama zaidi,vilevile mfumo huu umesaidia kuokoa muda wa kuwahudumia wananchi lakini pia hupunguza gharama za kutengeneza mifumo midogo midogo ya TEHEMA inayounganisha na mifumo ya taasisi nyingine,"amesema Mhandisi Ndomba.
Kuhusu Mfumo wa TeSWS,Ndomba amesema kuwa e-GA imeshirikiana na taasisi nyingine za umma ikiwemo TRA,TPA na Wizara ya fedha katika kusanifu mfumo huo wa pamoja mpango utakaoboresha mazingira ya biashara nchini na kuwezesha wafanyabishara kukamilisha maombi ya vibali na maandalizi ya malipo ya kodi za forodha kidijitali bila kwenda kwenye taasisi mbalimbali za udhibiti wa forodha hivyo kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo Mtendaji wa e-GA amezungumzia ubadilishaji wa taarifa kati ya mifumo ya TEHAMA ya serikali na ya sekta binafsi ambapo amesema unawezeshwa kadri ya mahitaji yanavyojitokeza.
Ametolea mfano mfumo wa malipo ya Serikali (GePG) kuwa umeunganishwa na Benki zote nchini pamoja na kampuni zote za simu za mkononi ili kuwezesha huduma za malipo ya Serikali kupitia simu na kwamba Mamlaka hiyo ipo tayari kufanya kazi na Taasisi zote za Umma kuhakikisha zinajiunga na kubadilishana taarifa kupitia GoVESB.