KITUO CHA UMEME LEMGURU ARUSHA KUANZA KAZI MUDA WOWOTE

 

Mwonekano wa nje wa kituo Kituo cha  kupoza umeme wa mradi wa Kenya Tanzania cha Lemguru kilichopo Mkoani Arusha kilichojengwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB). 
Mwakilishi Mkuu wa JICA, Ara Hitoshi  akizungumza na waandishi wa habari, Wakati Wa ziara ya wana habari Jijini Arusha kwenye mradi wa vituo vya kupoza umeme mradi wa Kenya Tanzania cha Lemguru. 
Afisa utawala na Mawasiliano JICA Tanzania, Alfred Zacharia akipewa maelekezo kutoka kwa Meneja mradi wa vituo vya kupoza umeme mradi wa Kenya Tanzania,  Timothy Mgaya,  Jijini Arusha. 






Picha mbalimbali za muonekano wa ndani wa Kituo cha Umeme Lemguru kilichopo Mkoani Arusha. 

Picha ya pamoja Kati ya viongozi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) na Viongozi wa Mradi wa Kituo cha Umeme Lemguru kilichopo Mkoani Arusha. 

  (PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY) 
                       
***********
  Na James Salvatory

 Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kimefanikiwa kujenga Kituo cha Umeme Lemguru kilichopo Mkoani Arusha kwa zaidi ya Sh655 bilioni. 
 
Akizungumza na waandishi wa habari, waliofanya ziara eneo hilo, Meneja mradi wa vituo vya kupoza umeme mradi wa Kenya Tanzania ,  Timothy Mgaya, amesema hadi sasa ujenzi wa miundombinu ya kituo hicho umefikia takribani asilimia 99 na kinachofanyika sasa ni uthibitishaji wa vifaa vilivyofungwa kwa kuvipima kabla ya kuwashwa rasmi. 
 
Amesema kukamilika kwa mradi huo utawezesha Tanzania kuwa na uwezo wa kununua umeme pindi kutakapokuwa na upungufu nchini na watu wa nchi za kusini wataweza kutumia mradi huo kupitisha umeme wao pindi wanapohitahi kununua Umeme kwa ajili ya nchi zao.
 
"Hii ni njia muhimu kwa nchi kwani itaweza kutusaidia katika namna zote, tukihitaji kununua umeme itakuwa rahisi au nchi za kusini zikitaka kununua umeme zitatumia njia yetu kwani watakapohitaji kupitisha watalipia," amesema Mgaya.


Mradi huo wa kusafirisha umeme unaounganisha Tanzania na Kenya kwa msongo wa Kilovoti 400 pia utakuwa na uwezo wa kusafirisha MW2,000.
 
Mgaya amesema lengo la mradi huo ni kusafirisha umeme kwa kushirikiana na Kenya kupitia East Afrika Power pool hadi Ethiopia sehemu wanayotegemea umeme huo kutoka na kwa upande wa kusini mradi huo ukiiunganisha Tanzania na Zambia kupitia South African Power Pool.
 
Katika upande wa uthibitishaji wa miundombinu unaofanyika sasa kabla ya mradi kuwashwa Mgaya alisema njia ya kutoka Singida hadi Arusha imeshathibitishwa baada ya kupimwa na kuwa tayari kwa matumizi.
 
"Njia iliyobakia ni Km114 kutoka Arusha hadi mpaka wa Namanga ambao uko hatua za kuthibitishwa vifaa hivyo kwa kupimwa na kuwa tayari kwa matumizi," amesema Mgaya.
 
Tanzania inakamilisha mradi huu wakati ambao tayari Kenya imeshaanza kununua umeme kutoka Ethiopia kwa mkataba wa miaka 25 tangu Novemba mwaka jana.
 
Mkataba huo uliosainiwa baina ya nchi hizo mbili uliifanya Ethiopia kuiuzia Kenya Megawati 600 kutoka mradi wao wa umeme wa Megawati 2,000 wanaozalisha kwa maji.
 
Mbali na Kenya, nchi nyingine zinazonunua umeme kutoka Ethiopia ni Sudan na Djibouti.
 
Akifafanua zaidi kuhusu mradi wa Kenya- Tanzania amesema unahusisha ujenzi wa kilomita 510 wa njia za kusafirisha umeme kwa msongo wa Kv400 kuanzia Singida hadi Arusha kabla ya kufika Kenya kituo cha Isinya.
 
Mradi huo una urefu wa Km414 kwa upande wa Tanzania huku ukiwa na urefu wa Km96 kwa upande wa Kenya.
 
Kwa upande wake Ofisa wa Mambo ya nje daraja la pili Ubalozi wa Japan, Tabochi Tomoyoshi amesema Japan kwa muda mrefu imekuwa ikiisaifia Tanzania katika utekelezaji wa shughuli za nishati huku akieleza kuwa mradi huo ni muhimu katika kufanya maendeleo ya nchi.
 
"Japan tunaheshimu sana umiliki wa shughuli zote chini ya mikono ya Afrika na katika ujenzi huu tunashirikiana na AfDB na tunatumaini kama nchi tutaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi mbalimbali," amesema Tomoyoshi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post