KATIBU wa Itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi CCM Mhe.Paul Makonda amewataka watendaji wa serikali kujitathmini kwa nafasi walizopewa kwa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo pasipokumuangusha Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kumuwakilisha kwenye kuhudumia wananchi.
Ameyasema hayo leo Desemba 21, 2023 Jijini Dar es Salaam, wakati akitoa tathmini ya ziara mbalimbali zilizofanywa na viongozi wa Chama hicho ili kuzungumza na wananchi na kujua changamoto zinazowakabili.
Amesema katika ziara hizo wameweza kuibua kero mbalimbali ambazo wanakutana nazo wananchi katika maeneo yao.
“Hizi ziara tumezifanya kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini na tumepata kero nyingi sasa niwaombe watendaji ambao mmewekwa kumsaidia Rais mjitathmini Je? mnafaa kuwepo mlipo na Je? mnatimiza matakwa ya Rais wetu katika kuwahudumia wananchi”. Amesema Makonda.
Sambamba na hayo Makonda amewataka watendaji wa shirikia la umeme TANESCO kutoa taarifa ya changamoto ya umeme wakiwa site na sio ofisini ili wananchi waweze kuelewa nini wanachozungumza.
Aidha makonda amewataka wananchi kujitokeza kutoa maoni yao kwenye dira ya maendeleo ya mwaka 2025-2050 ili iweze kutoa dira kwa serikali katika kupanga maendeleo na sera zake.
Katibu wa Itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi CCM Mhe.Paul Makonda akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 21,2023 katika Ofisi ndogo za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Lumumba Jijini Dar es Salaam