OSHA YAAGIZWA KUSAJILI MAENEO YOTE YA KAZI NCHINI IFIKAPO JUNI 2024

Katibu Mkuu – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza na wajumbe wa Baraza la OSHA katika Kikao cha Kwanza cha Baraza la Tano la Wafanyakazi kinachofanyika Mkoani Arusha tarehe 14 na 15 Mwezi Disemba 2023.

**************

Na Mwandishi Wetu

Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umeagizwa kusajili maeneo yote ya kazi nchini pamoja na kuhakikisha kwamba maeneo hayo yanapatiwa miongozo ya namna ya kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi vya magonjwa na ajali hadi kufikia Juni 2024.

Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhandisi Cyprian Luhemeja, alipokuwa akizundua Baraza la Tano la Wafanyakazi wa OSHA Jijini Arusha.

Mhandisi Luhemeja amesema OSHA imepewa dhamana ya kujenga nguvukazi salama na yenye afya njema kwa maendeleo endelevu ya Taifa na hivyo ni lazima Taasisi hiyo itimiza wajibu huo ipasavyo.

“OSHA ni Taasisi yetu ambayo imepewa jukumu la kusimamia Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ambayo serikali yetu kupitia Bunge iliitunga na kuunda chombo mahsusi ili kiweze kusimamia sheria hiyo kwa manufaa ya Watanzania. Hivyo, kama sehemu ya utekelezaji wa sheria hiyo nimewaagiza OSHA kuhakikisha kwamba maeneo yote ya kazi ambayo hayajasajiliwa wanayasajili na kuyafikishia huduma za usalama na afya,” amesema Katibu Mkuu Luhemeja na kuongeza:

“Suala la usalama na afya mahali pa kazi ni muhimu sana kwasababu dunia inabadilika kwahiyo OSHA kama chombo chetu rasmi kisimamie wafanyakazi wetu wasipate matatizo mbali mbali kazini. Pia, OSHA watoe elimu kwa waajiri kwamba suala la usalama na afya kwa wafanyakazi sio suala la hiari bali ni jambo la lazima katika maeneo yote ya kazi nchini.”

Akizungumza baada ya uzinduzi wa baraza hilo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema Taasisi yake imeyapokea maagizo ya Katibu Mkuu na itayatekeleza ipasavyo.

“Kikao chetu cha baraza hili kinalenga kufanya tathmini ya utendaji wetu kwa mwaka wa fedha uliopita (2022/2023) pamoja na nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2023/2024 hivyo kupitia kikao hiki ambacho kinajumuisha wawakilishi wa wafanyakazi wa kada zote tutakwenda kujadili namna bora ya kutekeleza maagizo tuliyopewa pamoja na kuendelea kuboresha utendaji wa Taasisi yetu,” ameeleza Kiongozi huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA.

Uzinduzi wa Baraza hilo la tano la wafanyakazi wa OSHA umefanyika sambamba na uchaguzi wa viongozi pamoja na wajumbe wa Kamati Tendaji ya Baraza hilo ambapo viongozi mbali mbali wakiwemo Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Comrade Heri Mkunda, Kamishina wa Kazi, Bi. Suzan Mkangwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Sarah Rwezaura.

Katibu Mkuu wa TUCTA ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TUGHE, Comrade Mkunda, ameipongeza Taasisi ya OSHA kwa kutekeleza ipasavyo Mkataba wa Mabaraza ya Wafanyakazi na hivyo kuwa kati ya Taasisi 20 zenye mabaraza bora nchini.

“Ni utaratibu wa kisheria kwamba Taasisi zote lazima ziwe na mabaraza ya wafanyakazi ili kutoa fursa kwa wafanyakazi kushiriki katika maamuzi muhimu yanayoihusu Taasisi yao kwani wafanyakazi ndio wamiliki wa Taasisi. Nitoe rai kwa waajiri wengine kuhakikisha mabaraza ya wafanyakazi yanakuwepo na yanafanya kazi ipasavyo kama ilivyo kwa OSHA na Taasisi nyingine zinazofanya vizuri.

OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) yenye jukumu la kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 iliyoundwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba taratibu muhimu za kulinda afya na usalama wa wafanyakazi zinazingatiwa ipasavyo.

Kamishna wa Kazi - Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu),Bi. Suzan Mkangwa akitoa salamu kwa wajumbe wa baraza la OSHA katika Kikao cha Kwanza cha Baraza la Tano la Wafanyakazi kinachofanyika Mkoani Arusha.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi Khadija Mwenda akiainisha ajenda za Kikao cha Kwanza cha Baraza la Tano la Wafanyakazi kwa wajumbe wa baraza hilo Mkoani Arusha.

Katibu Mkuu – Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu), Mhandisi. Cyprian Luhemeja akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mkatabata wa kuunda Baraza la Wafanyakazi uliosainiwa hivi karibuni kati ya OSHA  na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE).kushoto kwake ni Katibu Mkuu wa TUGHE, Bw. Hery Mkunda, kulia kwake ni Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda.

Baadhi ya Wajumbe wa Baraza la OSHA wakifuatilia hotuba za viongozi mbalimbali wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Kwanza cha Baraza la Tano la Wafanyakazi  Mkoani Arusha.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa OSHA wakiimba wimbo wa mshikamano wakati wa ufunguzi wa kikao cha baraza hilo Mkoani Arusha

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post