TGNP YATOA MAFUNZO YA KUANDIKA SHUHUDA ZA KUPIGANIA UKOMBOZI,HAKI NA USAWA KWA MAKUNDI MBALIMBALI.


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) umetoa mafunzo kwa Wanaharakati wa jinsia yenye lengo la kusaidia kuandika shuhuda zao kama kumbukumbu ya matokeo wanayoyapata wanapokuwa kazini ili yatumike kuwafunza watu wengine.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo leo Desemba 27,2023,Mshauri Elekezi wa masuala ya Maendeleo, Tathmini na Ufuatiliaji, Bw. Edson Nyingi amesema kuwa TGNP imeona kuna haja ya kuandika kuweka kumbukumbu nzuri na ya kudumu na kuachana na masimulizi pekee kwa njia ya mdomo ili kuweka kumbukumbu.

"Wadau wengi wa maendeleo wanafanya kazi na matokeo yanapatikana lakini hapakuwa na namna ya kuweka kumbukumbu za kudumu za matokeo ya kazi hizo hilo lilionekana swali huko mwanzoni na sasa hivi liko katika utekelezaji wa kazi za TGNP kuhakikisha inawajengea uwezo wadau wake kwa matokeo wa kazi wanazo zifanya", Bw. Nyingi amesema

Aidha ameeleza kuwa wanahitaji kuona matokeo ya kazi wanazo fanya wadau wa TGNP ili kuona jitihada na harakati za kumkomboa mwanamke ili kuwa na usawa katika masuala ya mgawanyo wa rasilimali na umiliki wa mali.

"Hii Warsha imelenga katika kuwasaidia wadau kuweza kufatilia taarifa zinazotokana na hiyo mifumo inayoleta usawa,inayoleta uwiano,katika masuala ya kijinsia huko kwenye jamii wanakofanya kazi ili kuyafanya sio tu yawe katika kumbukumbu zao ili yatumike kuwaeleza wengine ili wajifunze kutokana na matokeo ya kazi zao"Bw.Nyingi ameeleza.

Amesema kuna matokeo sasa yanayoonekana kutokana na kazi za Wanaharakati wa jinsia wa TGNP Sasa hivi wanaume wanaongozana na wake zao kwenda kliniki wanapokuwa wajawazito inatokana na harakati za TGNP za muda mrefu za kuleta usawa na uwiano wa majukumu katika familia.

Kwa upande wake, Mwanaharakati wa jinsia kutoka Mkoa wa Kilimanjaro shirika la Kisonge Community Development Organization Bi. Aika Manase ameishukuru taasisi ya TGNP kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo ynakwenda kusaidia kuweka kumbukumbu za kazi inayofanyika katika maandishi ambapo itachagiza kwa kiasi kikubwa kuweza kuishawishi serikali kuanzia ngazi ya jamii Hadi serikali kuu kuhusiana na mambo yaliyo jikita katika mlengo wa kijinsia.

"Kwa kweli ninalishukuru sana shirika la TGNP kwa kuandaa mafunzo haya yamekuja wakati sahihi sisi kama mashirika kwanza tulikua tunafanya kazi nzuri tulikua tunawasimulia watu kwa njia ya mdomo lakinj mafunzo haya yatatusaidia Kama wadau wa maendeleo kuweka Katika maandishi na kuweza kuishawishi serikali katika mambo yanayo husu Jinsia", Bi.Aika amesema.

Bi.Aika mesema sababu ambayo imesabisha kipindi cha nyuma wasiweke kazi zao katika maandishi ni uelewa mdogo ameeleza kwamba kutokana na mafunzo wanayo pewa itawasaidia kuweza kuandika kumbukumbu hata inapotokea mdau wa jinsia amepotezaa maisha wataweza kubaki wengine na kumbukumbu iliyopo kwa njia ya maandishi.

Naye Dereva Bajaji kutoka katika makundi yanayopigania Ukombozi,Haki na Usawa wa wanawake Bi. Husna Said ameeleza kuwa wamepata mafunzo ambayo yataweza kumsaidia kuandika hadithi kwa ajili ya kumbukumbu ya kazi ambayo ameifanya katika jamii ambayo itatumika Kama chachu ya mabadiliko kwa watu wengine.

Mafunzo hayo yatakuwa kwa siku nne kuanzia leo Desemba 27-30,2023 ambapo yamehusisha, Mashirika,Makundi na watu wanaotetea Ukombozi,haki na usawa wa wanawake nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post