Na Dotto Kwilasa,Dodoma
Ikiwa ni Siku ya kilele cha Wiki ya mlipa Kodi,Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Mkoa wa Dodoma imeadhimisha siku hiyo kwa kurudisha shukrani kwa jamii ambapo imetembelea vituo vya watoto yatima na makazi ya wenye mahitaji maalumu ili kuwafariji.
Aidha TRA imetembelea Hospitali ya Taifa ya afya ya akili Jijini hapa (MIREMBE) pamoja kituo cha watoto yatima cha Nyumba ya Matumaini kilichopo Miyuji Dodoma na kujitolea zawadi mbalimbali zikiweno Nguo, Sabuni, juisi,Viatu, Sukari, Unga na matunda kama shukurani kwa walipa kodi.
Akizungumza kwenye kilele hicho leo Desember 5,2023 jijini hapa, Meneja wa TRA Mkoa wa Dodoma,Castro John amesema wamefikia uamuzi huo ili kurudisha shukrani kwa jamii kutokana na umuhimu wa jamii kwenye maendeleo ya taifa.
Amesema,"Tunaunga mkono juhudi za kuwajenga wenye Uhitaji,tumekuja hapa kuwapa moyo ili wapone warudi kwenye uzalishaji na Sisi tupate Kodi,nawashukuru wateja wetu kwa kuendelea kutoa ushirikiano mzuri kwetu,tunatambua mchango ambao wameutoa kwa serikali na maendeleo ya mkoa huu kwa mwaka wa fedha 2022/23 ,"amesema na Ku ongeza;
"Tumetoa msaada huu kwa Wagonjwa wa afya ya akili kwa kuwa tunatambua wao ni sehemu ya Jamii kwa kuwa wagonjwa hao ni jamii ambayo inategemewa kiuchumi, " amesema.
Amesema TRA inajivunia kuwahudumia walipa kodi na wafanyabiashara kwani ndiyo wanaochochea maendeleo na kuwaomba walipa kodi wote kutumia machine ya EFDs kuweka kumbukumbu na kupata makadirio ya kodi sahihi.
"EFDs inasaidia kulipa kodi inayostahili kwani wengine wanakuwa wanasema kodi ni kubwa na wakati hawana kumbukumbu hivyo nawasihi walipa kodi kuhakikisha wanatumia mashine hiyo" amesisitiza
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Hospital ya MIREMBE Dr Innocent Mombeki amesema Masauala ya afya ya akili hapo nyuma hayakupewa kipaumbele lakini sasa kila mtu anaelewa umuhimu wa afya ya akili hivyo ni muhimu jamii kuendelea kutilia mkazo suala LA afya ya akili.
"Hakuna afya bila afya ya akili, akili yako ndo inakufanya uonekane binadamu, mtu akiwa na afya njema ndiye anakuwa mlipa Kodi mzuri
Naye Afisa ustawi wa Jamii wa Hosptali hiyo Faraja Mazengo ametumia nafasi hiyo kuiomba jamii na Wadau mbalimbali kusaidia huduma za afya katika hospitali hiyo kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya Wagonjwa wa afya ya akili ambao wamekuwa wakitelekezwa.
Amesema Hospitali hiyo ambayo kwa mwezi inapokea wagonjwa 700 hadi 800 imekuwa ikiwahudumia wagonjwa hao huku kukiwa hakuna msaada unaokidhi mahitaji hivyo kwa kujitoa zaidi kutasaidia kuwapa unafuu.
"Tumefarijika kuona TRA inatukumbuka,jamii inapaswa kuelewa kuwa huduma za Kodi zinategemea afya ya akili tunategemea kulipa kodi ikiwa tuko sawa kiakili hivyo ni muhimu kuwahudumia wenye uhitaji, " amesema