Wanafunzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM,)wanatarajia kupata fursa ya mafunzo ya Ubunifu na Ujasiriamali kutoka Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA) yatakayowasaidia wanafunzi hao kunufaika bunifu zao.
Mafunzo hayo maalum ya ubunifu yanatarajiwa yatakayoendeshwa kuanzia Desemba 4 hadi 8 mwaka huu na wakufunzi kutoka Japan kwa njia ya mtandao ili kuwapatia ujuzi wanafunzi hao ambao baadaye watashiriki mafunzo kwa vitendo katika viwanda mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, kuhusiana mafunzo hayo Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania Ara Hitoshi, amesema Shirika Hilo limekuwa likisaidia Serikali na wananchi katika nyanja mbalimbali na kuanzia mwaka jana wamekuwa wakishirikiana na UDSM katika nyanja ya ubunifu.
Hitoshi amesema,Seriksli ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA,) wameendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kufikia malengo katika sekta ya Elimu ambapo kupitia Program ya JICA Chair (Program for Japanese Studies) biashara vitendo na ubunifu vinahitajika.
Amesisitiza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa sekta binafsi katika Nchi zinazoendelea hivyo mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa vijana katika kuongeza idadi ya sekta binafsi hali itakayochagiza ukuaji wa uchumi kwa Taifa, kuongezeka kwa ajira na kukuza jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Ubunifu na Ujasiriamali ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam Prof. Hannibal Bwire amesema JICA kupitia program hiyo wamekuja kusaidia jitihada za kuwapatia vijana maarifa juu ya masuala ya ubunifu na ujasiriamali ili wakihitimu waweze kujiajiri na kuajiriwa.
"Kupitia kongamano la ujasiriamali lililofanyika Februari mwaka huu na watu zaidi ya 600 wakishiriki, Japan walieleza namna walivyomove kutoka katika vita kuu ya dunia hadi kufikia Dunia ya kwanza ya maendeleo kama inavyofahamika.
wamekuja kusaidia jitihada za UDSM kupitia mafunzo ambayo makundi matatu kati ya sita yatachaguliwa na yatatekeleza mawazo ya ubunifu na ujasiriamali kwa vitendo ndani ya wiki sita." Amesema Bwire
Naye Mratibu wa Ujasiriamali kutoka Kurugenzi ya Ubunifu na Ujasiriamali ya Chuo kikuu cha Dar es Salaam Dr. Winnie Nguni amesema, Program hiyo imelenga kusaidia wanafunzi kufikiri bunifu zao katika mlengo wa kibiashara.
"Tumegundua kuwa wanafunzi wengi wana uelewa na ujuzi sana ufundi wa kutengeneza bidhaa na wanakosa ujuzi, uelewa na maarifa ya kubiasharisha bidhaa zao...kupitia program hii tunaamini wanafunzi wengi zaidi watapata maarifa ya namna bora ya kufikia malengo yao na kufanikisha mawazo yao kibiashara." Amesema Nguni.