Na Mwandishi wetu _ Malunde 1 blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme ameweka jiwe la msingi kwenye jengo jipya la ofisi za halmashauri ya Msalala wilayani Kahama ujenzi uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 4.
Zoezi hilo la uwekaji wa jiwe la msingi limefayika leo Desemba 12, 2023 kwenye jengo jipya la ofisi za halmashauri ya Msalala lililopo kata ya Segese ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Shinyanga ikiongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Christina Mndeme kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa ndani ya wilaya ya Kahama.
Akizungumza
mara baada ya zoezi hilo Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amezitaka
halmashauri ya Ushetu, Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga na Manispaa kuiga
mfano na hatua hizo za ujenzi kwa ajili ya ofisi za watumishi na kuipongeza halmashauri ya Msalala kwa hatua za ukamilishaji wa jengo hilo la ofisi za halmashauri.
“Moja ya
malengo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuboresha mazingira ya
kufanyia kazi kwa watumishi, ni kweli mlikuwa mkifanya kazi katika mazingira magumu lakini
kwa sasa historia imeandikwa ndani ya halmashauri hii hongereni sana, kukamilisha
jengo hili ni hatua moja hatua inayofuata ni utoaji wa huduma bora kwa wananchi,
tuboreshe zaidi utoaji wa huduma bora kwa wananchi, lakini kupitia jengo hili
mipango mizuri yenye manufaa ndani ya halmashauri hii ipangwe kwenye jengo hili
na kuleta mabadiliko chanya kwa wakazi wa Msalala”, amesema RC Mndeme.
“Na kupitia jengo hili natoa maelekezo kwa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga, Ushetu na wilaya ya Shinyanga waige hatua hizi, ninyi mmekuwa mfano wa halmashauri zingine kwa sababu bado wanasuasua na hasa Shinyanga DC na Manispaa, lakini niwapongeze kwa kutumia samani za ndani zilizotengenezwa ndani ya mkoa huu hatua hii ni uungaji mkono wa shughuli zinazofanywa na wajasiriamali wazawa”, ameongeza RC Mndeme.
Muonekano wa Nje wa jengo la ofisi za halmashauri ya Msalala.
Zoezi la uwekaji wa jiwe la msingi likiendelea.
Mwenyekiti
wa halmashauri ya Msalala Mibako Mabubu ameipongeza serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi
wa jengo hilo la ofisi kwa ajili ya watumishi na kuongeza motisha kwa watumishi
wa halmashauri hiyo.
Aidha
kamati hiyo iliyoongozwa na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme
imetembelea kwenye miradi mbalimbali ikiwemo kutembelea na kukagua kituo cha
afya Bugarama, ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya sekondari ya wasichana ya
Bulyanhulu uliogharimu shilingi milioni 851, mradi wa shule ya msingi na sekondari Kabale pamoja na kutembelea mradi wa usambazaji umeme
vijijini uliopo kijiji cha Bumva kata ya Segese ambapo mpaka sasa vijiji 16
kati ya 68 vimefikiwa na huduma ya umeme.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga akiweka jiwe la msingi kwenye jengo la ofisi za halmashauri ya Msalala.
Social Plugin