Amesema hayo leo Desemba 11, 2023 katika ziara yake ya kikazi alipofika kuzindua mradi wa usambazaji umeme katika vijiji 17 kwenye kata ya Igunda Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mkandarasi kutoka Shirika la usambazaji umeme Tanzania TANESCO Antoni Tarimo amesema mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 64 huku kaya 699 zimeunganishiwa nishati ya umeme mpaka sasa.
“Mnamo Oktoba 2021 wakandarasi hawa walisaini mkataba wakufikisha umeme katika vijiji 146 vya wilaya ya Kahama ukiwa na gharama za utekelezaji Bilioni 32.8 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 64 za utekelezaji huku jumla ya vijiji 13 vipo kwenye hatua ya mwisho kukamilika, vijiji 58 kazi inaendelea na kaya 699 zimeunganishwa na huduma ya umeme mpaka sasa, mradi huu unatarajia kumalizika ifikapo Desemba 31, 2023”, amesema Antoni Tarimo.
Akieleza hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme katika kijiji cha Zobogo mwenyekiti wa kijiji hicho Sumuni Muhangwa amesema zipo baadhi ya taasisi ikiwemo za kidini kukosa huduma ya umeme kutokana na uchache wa nguzo zilizopo na kuiomba serikali kuongeza nguzo za kusambazia umeme kwenye kijiji hicho cha Zobogo.
“Tunashukuru sana siku ya leo kwa kuja kutuwashia umeme katika kijiji chetu, tunaipongeza sana serikali kwa kutuona wanakijiji wa kijiji cha Zobogo lakini tungeomba kuongezewa nguzo kwa sababu mpaka sasa yapo baadhi ya maeneo mbayo hayajafikiwa na huduma hii kutokana na uchache wea nguzo za kusambazia umeme ikiwemo makanisa na sehemu zingine”, amesema Sumuni Muhangwa.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la ushetu Emmanuel Cherehani amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwaajili ya utekelezaji wa mradi huo pamoja na miradi mingine inayoendelea kutekelezwa ndani ya halmashauri ya Ushetu.
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme amemtaka mkandarasi kuongeza kasi ya ukamilishaji wa mradi huo hadi ifikapo Desemba 31, 2023 awe ameshamaliza kusambaza umeme kwenye vijiji vyote 146.
“Umeme vijijini ni utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi na leo tumeshuhudia tangu tumepata uhuru leo wakazi wa kijiji hiki wananufaika na huduma ya umeme, wote tumesikia kwenye taarifa ya utekelezaji wa mradi huu vipo vijiji ambavyo bado havijafikiwa na huduma hii ya umeme, maelekezo yangu kwako mkandarasi ifikapo Desemba 31, 2023 uwe umekwisha sambaza umeme kwenye vijiji vyote 146 vilivyopo ndani ya wilaya ya Kahama kama mkataba unavyoelekeza, usipomaliza vijiji hivyo hatua zingine zitafuata”, amesema RC Mndeme.
Aidha Rc Mndeme ametembelea miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa ofisi za halmashauri ya Ushetu unaotekelezwa katika kata ya Nyamilangano uliogharimu takribani shilingi bilioni 5, ujenzi wa kituo cha afya Ushetu kilichopo kijiji cha Mbika kata ya Ushetu pamoja na ujenzi wa kituo cha polisi kata ya Ulowa.
Social Plugin