Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WANACHAMA EAC KUTHAMINI MCHANGO WA SEKTA ISIYO RASMI



Na; Mwandishi Wetu - Bujumbura, BURUNDI

Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameendelea kuthamini mchango unaotolewa na sekta isiyo rasmi katika kuleta maendeleo ya nchi hizo ikiwamo kukuza ajira.

Kauli hiyo imetolewa na Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Brigedia Jenerali Salum Mnumbe wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Tanzania yaliyofanyika leo tarehe 10 Desemba 2023 jijini Bujumbura, Burundi ikiwa ni sehemu ya shughuli za Maonesho ya 23 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Nguvu Kazi/ Jua Kali) yanayoendelea jijini humo.

Amesema kuwa nchi Wanachama wa jumuiya hiyo zilianzisha maonesho hayo kwa kutambua na kuthamini mchango unaotolewa na sekta isiyo rasmi katika kukuza maendeleo ya nchi hizo ikiwemo kuzalisha fursa za ajira kwa wingi na kuzalisha bidhaa zinazotumiwa zaidi na wananchi.

“Lengo la kuanzisha maonesho hayo lilikuwa ni kuwapatia fursa wajasiriamali ili waweze kushiriki kwa wingi katika shughuli za uzalishaji na kuwawezesha kukua zaidi” amesema Brig. Jen. Mnumbe

Vile vile, amewataka kuongeza bidii katika kuzalisha bidhaa bora kwa viwango vya kimataifa na kuzitangaza bidhaa hizo ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuongeza wigo wa soko na kuwasihi kushirikiana, kubadilishana ujuzi na masoko katika uzalishaji wa bidhaa na utengenezaji wa vifungashio na kuthaminisha.

Kadhalika, amepongeza wajasiriamali kutoka Tanzania kwa kuandaa bidhaa zenye ubunifu, ubora wa hali ya juu na zenye asili ya kitanzania.

Maonesho hayo ya 23 yamewashirikisha wajasiriamali 1,500 kutoka nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakiwemo 259 kutoka Tanzania yanafanyika kwa mara ya tatu nchini Burundi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com